John Pombe Magufuli, rais wa Tanzania kwa muhula wa pili
John Magufuli, amechukuwa hatamu ya uongozi wa nchi kwa muhula wa pili mfululizo, licha ya kuendelea kukosolewa na wapizani wake, wakimshtmu kuirejesha nchi hiyo katika zama za utawala wa kiimla.
Imechapishwa:
Magufuli ni rais wa Tanzania kwa muhula wa pili tangu Alhamisi wiki hii, baada ya kuapishwa mbele ya wabunge, viongozi mbalimbali kutoka baadhi ya mataifa barani Afrika, ikiwa ni pamoja na rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, Azali Assoumani wa Comoro na Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe.
Wengi wanahofu kwamba ushindi huu mkubwa wa John Pombe Magufuli, pamoja na ule wa chama tawala, ambacho kilipata viti 262 kati ya viti 264 katika Bunge, ni katika muendelezo wa kuminya demokrasia ya vyama vingi na utulivu ambavyo vimeifanya nchi hii kufikia sasa kuwa na maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Wapinzani wa Magufuli wanabaini kwamba rais huyo aliyechaguliwa tangu mwaka 2015, asingelishinda uchaguzi huo, lakini alipata ushindi huo baada ya kupewa kura ambazo hakustahili kupata.
Rais Magufuli aliibuka mshindi katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 28 kwa 84% ya kura.
Hata hivyo rais Magufuli alisifika kwa kukabiliana na ufisadi na kuimarisha uchumi wa nchi yake katika miaka yote mitano ya muhula wake wa kwanza..
Mshindi mwingine mkubwa katika uchaguzi huu ni CCM (Chama Cha Mapinduzi, Chama kilichotetea uhuru wa Tanzania), chama chake rais Magufuli. Chama hiki kiko madarakani bila usumbufu tangu uhuru wa nchi hiyo mnamo mwaka 1961. Chama hiki ambacho kinadaiwa kuwa kimewapoteza wafuasi wengi, kimepata karibu viti vyote 264 katika bunge la Tanzania.
CCM pia ilishinda kwa kiasi kikubwa katika visiwa vya Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Tanzania na hadi sasa imekuwa ikichukuliwa kama ngome ya upinzani.
Wakati huo huo vyama vya upinzani vilifutilia mbali matokeo hayo ya uchaguzi. Lakini kwa kuwa sheria ya Tanzania inakataza kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani, wapinzani waliwataka raia kuanzisha maandamano. Pia waliwasilisha kesi kwa Jumuiya ya Madola ambayo Tanzania ni mwanachama, wakiomba jumuiya hiyo kupinga hadharani uchaguzi huo, kutuma ujumbe na kusitisha uanachama wa nchi hiyo kwa jumuiya hii ya nchi zinazozungumza Kiingereza. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema "ina wasiwasi juu ya ripoti za kuaminika za kasoro za uchaguzi."