UGANDA-WINE-SIASA-USALAMA

Vurugu zatokea baada ya Bobi Wine kukamatwa Kampala

Mkosoaji mkubwa wa rais Museveni na mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine.
Mkosoaji mkubwa wa rais Museveni na mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine. France24

Kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine kumeleta ghasia na maandamano huko Kampala na miji mingine mikubwa wakati wafuasi wake wakitaka aachiliwe.

Matangazo ya kibiashara

Kyagulanyi alikamatwa dakika chache kabla ya kuanza kuhutubia mkutano wa hadhara wilayani Luuka kama kilomita 156 Mashariki mwa mji wa Kampala. Alipokamatwa, alipepelekwa katika kituo cha polisi cha Nalufeenya katika mji wa Jinja.

Makabiliano yalitokea pale polisi ilipokua ikijaribu kumdhibiti Robert Kyagulanyi, huku wafuasi wake wakitaka aachiliwe mara moja. Polisi ililazimika kufyatua risasi hewani na kutumia mabomu ya machozi kwa kuwatawanya waandamanaji.

Kukamatwa kwake kulizua maandamano jijini Kampala na miji mingine lakini polisi walikuwa wepesi kuzima moto na kutawanya waandamanaji

Mkurugenzi wa operesheni katika Polisi ya Uganda Edward Ochom amesema Kyagulanyi amekuwa akifanya mikutano ya kampeni kinyume na sheria badala ya kufanya mikutano ya watu 200 tu kama ilivyoagiza tume ya uchaguzi.

“Wacha wahakikishe kuwa hawana umati ambao unaweza kusababisha kuenea kwa COVID-19. Hatutakuwa na shida nao. Tume ya uchaguzi iliwaambia wagombea wote katika uchaguzi huokwamba ni marufuku kufanya mikutano ya hadhara, marufuku kufanya maandamano au kufungua magari yao. Kwa hivyo tatizo ni kwa sababu yeye hakufuata miongozo hii, ” amesema Edward Ochom.

Wakili wa Kyagulanyi, Anthony Wameli, amesema mteja wake amekamatwa kwa sababu ya siasa.

“Hajakiuka sheria yoyote, watu wanampenda tu. Oliona jinsi watu walivyogelea majini kwa kwenda kumsikiliza, huo ndio upendo kwa sababu ana ujumbe wa kuboresha nchi yetu. Watu wanampenda halafu viongozi serikalini wanamuogopa ” , amesema Anthony Wameli.

Kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi leo kumewaacha wafuasi wake wakiwa na hasira na kusababisha maandamano. Wakati polisi imewazuia, wanasubiri kuona ikiwa ataruhusiwa kuendelea na kampeni zake.