UGANDA-SIASA-USALAMA

Uganda: Kumi na sita wauawa katika siku mbili za vurugu baada ya Bobi Wine kukamatwa

Watu 16 wanaripotiwa kuwa wameuawa katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, ndani ya kipindi cha siku mbili za makabiliano yaliyozuka baada ya mpinzani maarufu nchini humo Bobi Wine kukamatwa, klingana na taarifaya polisi.

Mwanansiasa wa upinzani maarufu Uganda Bobi Wine, ambaye anaendelea kushikiliwa na polisi.
Mwanansiasa wa upinzani maarufu Uganda Bobi Wine, ambaye anaendelea kushikiliwa na polisi. AFP Photos/ Guillem Sartorio
Matangazo ya kibiashara

"Idadi ya waliopoteza maisha kufikia sasa ni 16 na 45 wamejeruhiwa, baadhi wakiwa katika hali mbaya," mkuu wa polisi wa jiji la Kampala Moses Kafeero amesema, na kuongeza kuwa "karibu watu 350 wamekamatwa kwa vitendo vya vurugu", hasa uporaji, uharibifu wa mali na wizi.

Robert Kyagulanyi maarufu Kama Bobi Wine bado anashikiliwa na polisi na mpaka sasa bado hajashtakiwa.

Wagombea urais kutoka vyama vya upinzani nchini Uganda wamesema kuwa wanasitisha kampeni zao hadi pale mgombea mwenzao Bobi Wine atakapoachiliwa huru.

Bobi Wine alikamatwa siku ya Jumatano, Mashariki mwa eneo la Luuka baada ya polisi kumshtumu kwa kosa la kusababisha mikusanyiko ya watu ikiwa ni uvunjaji wa miongozo ya kukabiliana na virusi vya Corona iliowekwa na Tume ya Uchaguzi.