KENYA-CORONA

Raia watakiwa kujiandaa na makali ya kodi na kupanda bei kwa bidhaa kuanzia mwakani

Bunge la taifa nchini Kenya
Bunge la taifa nchini Kenya Kevin MIDIGO / AFP

Msikilizaji wakati huu taifa la Kenya, likiendelea kukabiliana na janga la Corona pamoja na athari za kiuchumi kutokana na ugonjwa huo, sasa wananchi wanatakiwa kujiandaa kwa ongezeko la kodi na kupanda bei kwa bidhaa muhimi kama chakula na mafuta kuanzia mwakani wakati ahueni iliyokuwa imetolewa na Serikali itakapofikia tamati.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa fedha nchini Kenya, Ukur Yatani, juma hili alisema kodi inayotozwa kwenye mishahara kuanzia mwakani itarejea katika kiwango cha kawaida cha asilimia 30, kutoka asilimia 25 iliyopunguzwa na Serikali kutokana na janga la Corona.

 

Kodi hii ilipunguzwa ili kutoa ahueni kwa mamilioni ya wafanyakazi nchini humo ili waweze kukabiliana na changamoto za kiuchumi zilizosababishwa na Covid 19.

 

Serikali pia inatarajiwa kurejesha kodi ya thamani kwenye bidhaa kwa asilimia 16 kutoka asilimia 14 iliyokuwa imepunguzwa na Serikali ili kupunguza makali ya Corona.

 

Waziri yatani, amesema kurejesha tozo za awali kunalenga kuisaidia Serikali kuongeza ukusanyaji mapato.

 

Aidha waziri Yatani, amezitaka wizara na taasisi nyingine za Serikali kujiandaa na makali yatakayoshuhudiwa, ambapo Serikali inalenga pia kupunguza baadhi ya bajeti za wizara na taasisi ili kufidia ombwe lililopo sasa.

 

Haya yanajiri wakati huu kamati ya bunge ikitarajiwa kujadili ripoti ya uchunguzi kuhusu sakata la matumizi mabaya ya fedha za kukabiliana na janga la Corona katika ofisi ya manunuzi ya dawa za Serikali Kemsa.