KENYA-SOMALIA-DIPLOMASIA

Kenya yataka mvutano baina yake na Somalia kutatuliwa

Uhuru Kenyatta rais wa Kenya na mwenyeji wake Mohamed Abdullahi Farmajo walipokutana jijini Nairobi  Novemba 14 2019
Uhuru Kenyatta rais wa Kenya na mwenyeji wake Mohamed Abdullahi Farmajo walipokutana jijini Nairobi Novemba 14 2019 State House Kenya

Serikali ya Kenya imesema imeunda kamati maalum kutatua mvutano baina yake na Somalia, saa chache baada ya serikali ya Mogadishu kutangaza kusitisha uhusiano wa kidiplomasia na Kenya.

Matangazo ya kibiashara

Mapema siku ya Jumanne, tarifa kutoka mjini Mogadishu ilieleza kuwa nchi hiyo imesitisha uhusiano na Kenya na hivyo kuwataka wanadiplomasia wake waliopo jijini Nairobi, kurejea nyumbani, huku wale wa Kenya walio nchini Somalia wakipewa siku saba kuondoka nchini humo.

Waziri wa Habari wa Somalia, Osman Abukar Dubbe akitoa taarifa hiyo, ameishtumu Kenya kuendelea kuingilia masuala yake ya ndani, madai ambayo hata hivyo, seriklai jijini Nairobi imekuwa ikikanusha.

Kanali mstaafu Cyrus Oguna, msemaji wa serikali ya Kenya, amesema nchi hiyo haiwezi kuchukua hatua kama ilivyofanya Solamia na badala yake imeunda kamati kushughulikia mvutano unaoendelea.

Hatua ya Somalia imekuja, baada ya uongozi wa nchi hiyo kuiandikia barua Jumuiya ya maendeleo ya Afrika Mashariki na pembe ya Afrika (IGAD) kuilalamikia Kenya na viongozi wa nchi hizo watakutana tarehe 20 mwezi huu.

Mvutano huu unakuja wakati huu Somalia ikijiandaa kuwa na uchaguzi unaosubiriwa uliopangwa kufanyika mapema mwaka ujao.

Siku ya Jumatatu rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alikutana na kufanya mazungumzo na rais wa jimbo linalojitegemea na ambalo lilitangaza kujitawala la Somaliland Muse Bihi Abdi.

Uongozi wa Mogadishu pia umekuwa ukiishtumu Kenya kwa kumuunga mkono rais wa jimbo la Jubaland, Ahmed Madobe, ambaye ana uhusiano mzuri na rais wa nchi hiyo Mohamed Abdullahi Farmajo.

Mzozo huu unajiri wakati huu nchi hizo zikiendelea kutegemeana katika masuala ya kiuchumi pamoja na usalama kutokana na jeshi la Kenya, KDF, kuwa nchini Somalia kusaidia katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Al Shabab.