BURUNDI

Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya, afariki dunia

Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya.
Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya. RFI

Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya, amefariki dunia kwa ugonjwa wa Covidi 19, wakati akipatiwa matibabu jijini Paris, Ufaransa. 

Matangazo ya kibiashara

Buyoya ambaye majuma kadhaa nyuma alitangaza kujiuzulu nafasi yake kama mjumbe maalumu wa umoja wa Afrika kwa nchi ya Mali na ukanda wa Sahel, alianza kuugua akiwa jijini bamako, kabla ya kusafirishwa Ufaransa.

Buyoya alikuwa akituhumiwa na Serikali ya Burundi kwa kuhusika na mauaji ya rais wa zamani wa Burundi, Melchior Ndadaye.

Mmoja ya wanafamilia wake ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema "Alisafirishwa kwenda Paris jana mchana."

Buyoya alijiuzulu nafasi zake ndani ya umoja wa Afrika, baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kutokana na tuhuma za mauaji ya mtangulizi wake mwaka 1993.

Mapinduzi na Vita

Buyoya, ambaye ni mtusi, alitokea katika familia ya kipato cha kati ambapo alianzia jeshini kabla ya kuongoza taifa hilo kupitia mapindizi ya kijeshi ya mwaka 1987.

Wakati wa utawala wake, alifanya harakati za kurejesha demokrasia katika taifa lake, ambapo aliachia madaraka mwaka 1993 baada ya uchaguzi wa kwanza nwa kidemokrasia, ambapo alishindwa vibaya na Melchior Ndadaye, ambaye alikuwa Muhutu.

Hata hivyo wanajeshi wa Kitusi walimuua Ndadaye kwa kumpiga risasi miezi minne tu tangu aingie madarakani.

Mauaji yake yaliitumbukiza Burundi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya wahutu walio wengi na jamii ndogo ya Watusi.

Buyoya alirejea tena madarakani baada ya mapinduzi mengine na kuongoza taifa hilo kati ya mwaka 1996 hadi 2003.

Mwaka 2000 alitia saini mkataba wa amani wa Arusha, Tanzania, mkataba uliolenga kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambapo watu zaidi ya laki 3 waliuawa kati ya mwaka 1993 na 2006.

Buyoya aliachia madaraka mwaka 2003 kwa kufuata sharti la mkataba wa amani wa Arusha.

Kifo chake kinafuatia kile cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza, ambaye alifariki mwezi Juni mwaka huu akiwa na umri wa miaka 55 kutokana na kile Serikali ilisema shinikizo la moyo kabla ya kuibuka kwa taarifa kuwa alifariki kutokana na maradhi ya Covid 19.

Tofauti na viongozi wengine wa kikanda, Nkurunziza, alijinasibu kuwa nchi yake imeponywa kwa uwezo wa Mungu, lakini punde baada ya mtangulizi wake kuingia Jenerali Evarister Ndayishimiye, akatangaza ugonjwa huo kuwa adui namba moja wa nchi.