BURUNDI

Burundi: Pierre Buyoya, rais wa zamani mwenye urithi wa kutatanisha

Pierre Buyoya, rais wa zamani wa Burundi aliyefariki dunia 18.12.2020 nchini Ufaransa
Pierre Buyoya, rais wa zamani wa Burundi aliyefariki dunia 18.12.2020 nchini Ufaransa AP Photo/Keystone, Salvatore Di Nolfi

Rais wa zamani wa Burundi, aliyesafirishwa kutoka Mali kutokana na hali yake ya afya kuwa mbaya ghafla, baada ya kuambukizwa virusi vya Corona alifariki dunia baada ya kuwasili katika mji mkuu wa Ufaransa Paris Desemba 17.

Matangazo ya kibiashara

Pierre Buyoya amekuwa anaheshimiwa kwa jinsi alivyoachia ngazi na kukabidhi madaraka kwa rais  Domitien Ndayizeye, baada ya kuanzishwa kipindi cha mpito kabla ya uchaguzi wa mwaka 2005.

Hata hivyo ameacha hali ya sintofahamu nchini mwake, Burundi, baada ya kuhukumiwa na mahakama kifungo cha maisha kwa kuhusika katika mauaji ya rais aliyechaguliwa kidemokrasia Melchior Ndadaye, kutoka kabila la Wahutu, walio wengi nchini humo.

Mwaka 2014 Pierre Buyoya alizungumza "jambo muhimu sio jinsi unavyoingia madarakani, lakini ni jinsi unavyoiacha ngazi".

Licha ya kuheshimiwa kwake kote, Pierre Buyoya alikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wapinzani wake, wakati wa kampeni yake ya kumrithi Abdou Diouf kwenye wadhifa wa katibu mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya nchi zinazozungumza Kifaransa la Francophonie (OIF).

Afisa huyo wa zamani katika jeshi la zamani la FAB, mwenye cheo cha Meja, alihudumu mara mbili madarakani kwa jumla ya miaka 13 (mwaka 1987 na mwaka 1996) baada ya kuwapindua watangulizi wake.

Marehemu Pierre Buyoya aliingia madarakani kwa mwara ya kwanza kama rais baada mapundizi ya kijeshi dhidi ya utawala wa rais Jean-Baptiste Bagaza mwaka 1987 ambaye pia aliingia madarakani kwa mapinduzi dhidi ya mtangulizi wake Michel Micombero mwaka 1976.

Utawala wake wa miaka sita uligubikwa na mambo mbali mbali ambayo yalibadili sura ya nchi kama vile mauaji ya kinyama yaliyofanyika katika kitongoji cha Ntega-Marangara mwaka 1988, makubaliano ya umoja wa Warundi yaliyoidhinishwa mwaka 1991, kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1993, na mengine mengi.

Aliondoka madrakani mwaka 1993 baada ya kushindwa katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi kuwahi kufanyika tangu mwaka 1960. Wakati huo , mtangulizi wake Rais Melchior Ndadaye kutoka chama cha Frodebu ndiye aliyemshinda kwa asilimia zaidi ya 65% ya kura na Pierre Buyoya aliyekuwa wakati huo amegombea kwa tiketi ya chama cha Uprona aliibuka na 33% za kura.

Buyoya alirejea tena madarakani mwezi wa Julai 1996, baada ya kumpindua tena madarakani rais wa mpito Sylvestre Ntibantunganya, ambaye wakati huo alichukua madaraka kufuatia kifo cha Cyprien Ntaryamira ambaye alikufa katika ajali ya ndege pamoja na aliyekuwa rais wa Rwanda wakati huo Juvenal Habyarimana.

Mwaka 2008, aliteuliwa kuwa mjumbe maalumu wa amani Umoja wa Mataifa katika nchi ya Mali na Sahel kufuatia mzozo wa kivita uliokuwa ukitokota kati ya Mali na nchi jirani ya Sudan.

Mwezi wa Januari mwaka 2013, ndipo aliteuliwa tena na Umoja wa Afrika kama mjumbe maalumu katika nchi ya Mali na eneo la Sahel.

Uhasama kati ya Buyoyoa na utawala wa CNDD-FDD

Mambo yalibadilika kuanzia mwaka 2015,wakati ulipoibuka mzozo wa kisiasa kuhusiana na aliyekuwa rais wa Burundi hayati Pierre Nkurunziza, kugombea muhula wa tatu wa urais.

Wakati huo wapinzani wa serikali walisema kuwa hatua ya Nkurunziza ni kinyume cha sheria , lakini chama chake cha CNDD-FDD, walisisitiza kuwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa sheria.

Buyoya hakukubaliana na hatua ya Nkurunziza kugomea urais kwa muhula wa tatu akinukuu kuwa "makubaliano ya amani ya Arusha'' yanabainisha wazi kwamba rais anapaswa kuongoza kwa mihula miwili pekee.

Kutokana na kauli hiyo, uhusiano wake na utawala wa Nkurunziza uliharibika na hakuweza tena kukanyaga katika ardhi ya Burundi.

Mwezi Oktoba, alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani na mahakama ya Burundi kwa kosa la mauaji ya rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia nchini, Rais Melchior Ndadaye mwaka 1993 - ambayo yalisababisha mauaji ya karibu watu 300,000. Alikana kufanya makosa

Mwezi uliyopita, alijiuzulu kama mjumbe wa Muungano wa Afrika wa eneo la Sahel, na kusema kuwa anataka kutumia muda wake zaidi kusafisha jina lake.