BURUNDI

Wanahabari wanne wa Burundi, waachiwa kwa msamaha wa rais

Wanahabari wa Burundi, waliaochiliwa huru baada ya msamaha wa rais
Wanahabari wa Burundi, waliaochiliwa huru baada ya msamaha wa rais Tchandrou Nitanga / AFP

Wanahabari wanne wa Burundi, waliokuwa wamefungwa jela kwa mwaka mmoja baada ya kupatikana na makosa ya kutishia usalama wa nchi hiyo, mashtaka yalishtumiwa na wanaharakati wa haki za binadamu, wameachiliwa huru baada ya kupewa msamaha wa rais.

Matangazo ya kibiashara

Wanahabari hao Agnes Ndirubusa, Christine Kamikazi, Egide Harerimana na Terence Mpozenzi wafanyikazi wa Shirika la Habari la Iwacu, walikamatwa mwezi Oktoba mwaka 2019 katika mkoa wa Bubanzi walipokwenda kuripoti mapigano kati ya waasi na vikosi vya  serikali.

 

Kabla ya kuachiliwa huru, wanahabari hao walikuwa wamefungwa miaka miwili na nusu jela, hukumu ambayo ilishikiliwa na Mahakama ya rufaa mwezi Juni.

 

Mmoja wa wanahabari hao waliaochiliwa huru, Agnes Ndirubusa, amesema amefurahi sana kuondoka gerezani.

 

“Nafurahi sana kuona kuwa nimetoka gerezani, kilikuwa kitu kibaya sana kwangu na kwa familia yangu, nimefurahi sana kuondoka gerezani,” amesema.

 

Mwanzilishi wa Shirika hilo la Habari la Iwacu, Antoine Kubarahe amesema kuachiliwa huru kwa wanahabari hao ni faraja kubwa na ushindi katika vita vya uhuru wa Habari nchini humo.

 

“Wanahabari hawa wanNe, narudia, hawakuwa na kosa lolote, walikuwa wanafanya kazi yao,” amesema.

 

Msemaji katika Ikulu ya rais nchini humo Willy Nyamwite, amemwambia ripota wetu wa Bujumbura Juvenal Bigirimana kuwa, wanahabari hao waliachiliwa huru kwa msamaha wa rais Evariste Ndayishimiye.

 

“Napenda kuwakumbusha kuwa, watangazaji wanne walioachwa huru, waliandika barua na kumwomba rais awasamehe  na akawasamehe, walilipa faini zote lakini pia walionesha tabia njema wakiwa gerezani, na ndio sababu ya kusamehewa," amesema.

 

Mwezi Oktoba, kundi la mashirika 65 ya haki za binadamu kupitia taarifa ya pamoja, yalitoa taarifa ya pamoja wakitaka kuachiliwa huru kwa wanahabari hao.

 

Ripoti ya Shirika linalotetea haki za wanahabari duniani RSF, linaiorodhesha Burundi katika nafasi ya 160 kati ya 180 duniani katika uhuru wa vyombo vya Habari.