UGANDA

Joto la kisiasa lazidi kupanda nchini Uganda, Wine aonya wizi wa kura

Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, mgombea wa urais nchini Uganda
Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, mgombea wa urais nchini Uganda France24

Mgombea urais nchini Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu anayejulikana kwa jina maarufu Bobi Wine anayewania uongozi wa nchi hiyo kupitia chama cha upinzani cha NUP, amesema hatakubali udanganyifu wakati wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 14 mwezi huu.

Matangazo ya kibiashara

Kyagulanyi amemshtumu kiongozi wa muda mrefu nchini humo na mpinzani wake Yoweri Kaguta Museveni kwa kupanga njama za kuiba kura.

Museveni ambaye ameendeleza kampeni kuomba kuchaguliwa tena baada ya kuongoza kwa miaka thelathini, hivi majuzi ameeleza ni kwanini anawatumia wanajeshi kukabiliana na wafuasi wa Bobi Wine hasa jijini Kampala.

Miezi mitatu iliyopita wafuasi 132 wa Chama cha NUP kinachongozwa na Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine walifikishwa katika mahakama ya kijeshi kujibu mashtaka ya kupatikana na vitu vinavyodaiwa kuwa sare za jeshi.

Wafuasi hao walikamatwa wakati vikosi vya usalama vilipovamia makao makuu ya chama hicho na kutwaa kofia aina ya Bereti, mavazi mbalimbali na picha za Bobi Wine.

Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kwa jina la kisanii Bobi Wine, ni mwanasiasa, mfanyabiashara, mhisani, mwanamuziki na muigizaji nchini Uganda. Amekuwa mbunge wa Kyadondo Masahriki tangu Julai 11, 2017.

Bobi Wine alizaliwa Februari 12, 1982 katika hospitali ya Nkozi ambako marehemu mama yake alikuwa akifanya kazi. Wanachama wa familia yake wana asili yao katika iliyokuwa wilaya ya Mpigi, ambayo kwa sasa ni wilaya ya Gomba. Alikulia katika eneo la mabanda la Kamwokya, kaskazini-mashariki mwa Kampala, mji mkuu wa Uganda.

Mwaka 2017, Bobi Wine alitangaza kugombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kyadondo Mashariki na kuendesha kampeni ya nyumba hadi nyumba iliyowavutia watu wengi.

Alishinda uchaguzi huo kwa tofauti kubwa sana ya kura dhidi ya mgombea wa chama tawala cha NRM na pia mgombea wa chama kikuu cha upinzani cha FDC.

Mwaka 2018, Bobi Wine alizidi umaarufu, na kuongoza ushindi katika chaguzi kadhaa ndogo kwa wagombea aliowapigia kampeni, na hivyo kuwachachafya wagombea wa chama tawala pamoja na wale wa FDC.