BURUNDI

Burundi kufunga mipaka Jumatatu kudhibiti maambukizi ya Corona

Rais wa Burundi  Evariste Ndayishimiye
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye AFP Photos/Tchandrou Nitanga

Serikali ya Burundi imetangaza kuwa itafunga mipaka yake ya majini na ardhini kuanzia Jumatatu ijayo, ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona ambayo yameonekana kuongezeka wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii imekua, baada ya wiki hii watu zaidi ya 40 kuambukizwa virusi hivyo ndani ya siku mbili katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Aidha, serikali nchini humo imetangaza kuwa abiria wote watakaowasili nchini humo kwa ndege, watalazimika kukaa karatini kwa muda siku saba na watakaopatikana na virusi hivyo, watapelekwa katika vituo maalum kwa gharama zao.

Agizo hili jipya limetolewa na Waziri wa usalama Gervais Ndirakobuca, wakati huu nchi hiyo ikiwa na maambukizi 884 ya corona tangu kisa cha kwanza kilichoripotiwa mwaka uliopita.

Hata hivyo, wadadisi wa mambo wanasema kuwa huenda nchi hiyo ikawa na maambukizi makubwa kinyume na inavyoripotiwa wakati huu kutokana na idadi ndogo ya upimaji wa virusi hivyo.