UGANDA-UCHAGUZI

Polisi wadai Bobi Wine ana mpango wa kujiteka

Mgombea urais nchini Uganda kupitia upinzani  Bobi Wine
Mgombea urais nchini Uganda kupitia upinzani Bobi Wine France24

Kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini Uganda hapo kesho mitandoa ya kijamii imefungwa, huku maafisa wa usalama wakidai kuwa mgombea wa urais wa upinzani Bobi Wine anapanga kujiteka baada kupiga kura ili kuchochea vurugu.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa jeshi la polisi Fred Enanga amesema Bobi Wine hana mipango mizuri baada ya uchaguzi huo.

“Tuna habari za kuaminika kwa Robert Kyagulanyi anataka kujificha baada ya kupiga kura labda katika moja ya ubalozi wa nchi ya kigeni kisha baadaye aseme kuwa ametekwa ili wafuasi wake waanze fujo, tunamwonya asijaribu kufanya hivyo," amesema Enanga.

Ripoti ya Kenneth Lukwago akiwa jijini Kampala Januari 13 2021

Hata hivyo, madai hayo ya polisi yamekanusha na Bobi Wine, ambaye amesema inaonekana kuwa maafisa wa usalama wanataka kumzuia nyumbani kwake.

"Sina sababu ya kujificha. Nitakuwa hapa nyumbani kwangu. Labda wanataka kunizuia nyumbani kwangu na ndio sababu wanasema hivyo," alisema Bobi Wine.

Katika hatua nyingine, jeshi nchini humo limetete hatua yake ya kuwapeleka maafisa wake kwa wingi jijini Kampala na kukanusha kuwa kuna mpango wa kuwatisha wapiga kura.

“Nimesikia watu wengi wakisema kwamba kwanini wanajeshi ni wengi? Wametumwa kutokana na vitisho ambavyo tumepata. Hatuna mpango wa kumtisha yeyote," amesema Brigedia Flavia Byekwaso msemaji wa jeshi la UPDF.

Kuna hali ya wasiwasi hasa jijini Kampala, kuelekea Uchaguzi huu ambao ushindani mkubwa ni kati ya kiongozi wa muda mrefu Yoweri Museveni na mgombea kijana Bobi Wine.