UGANDA-UCHAGUZI

Raia wa Uganda wapiga kura, mtandao wa Interneti wazimwa

Wapiga kura nchini Uganda Januari 14 2021
Wapiga kura nchini Uganda Januari 14 2021 REUTERS/Baz Ratner

Wananchi wa Uganda wanapiga kura leo Alhamisi Januari 14 kumchagua rais wao mpya, ambapo ushindani mkubwa unatarajiwa kati ya rais anayemaliza muda wake Yoweri Kaguta Museveni na mwanamuzi maarufu Robert Kyagulanyi, anayejulikana kwa jina la kisanii la Bobi Wine.

Matangazo ya kibiashara

Mwanamuziki nyota wa pop aliye na umri wa mika 38, anachuana kisiasa na mmoja wa viongozi wa Afrika aliyehudumu muda mrefu madarakani katika uchaguzi wa Uganda unaokabiliwa na ushindani mkali

Wapigakura zaidi ya Milioni 17 wanatarajia kuamua kati ya wagombea hao yule ambaye atakuwa rais wao mpya.

Kampeni za uchaguzi ambazo zilimalizika siku ya jumatano wiki hii zilikumbwa na vurugu ambazo zilisababisha vifo vya watu kadhaa, wengi kutoka kambi ya upinzani.

Wakati huo huo mamia ya wanajeshi wameshika doria katika barabara za mji mkuu Kampala na miji kadhaa "kudumisha utulivu", mamlaka zimesema. Serikali inataka kuepuka vurugu zaidi, kama ile iliyoikumba nchi hiyo mnamo mwezi Novemba 2020.

"Kudumisha amani ni wajibu na sio huduma". alisema rais wa Uganda Yoweri Museveni siku Jumanne, baada ya kuagizwa kupelekwa magari ya kivita na mamia ya wanajeshi katika mji mkuu Kampala na miji mingine.

Mnamo mwezi Novemba, watu 54 waliuawa katika makabiliano na polisi, ambayo yalisababishwa na kukamatwa kwa kiongozi mkuu wa upinzani Bobi Wine.

Yoweri Museveni anawalaumu viongozi wa upinzani ambao anasema walihimiza waandamanaji vijana kufanya vurugu. Alhamisi hii, rais anasema hataki nchi yake itumbukie katika vurugu. Kwa hivyo ametoa wito kwa jeshi kutoa ulinzi mkali katika mji mkuu na polisi wachunguze kwenye paa za nyumba na majengo ili kukabiliana na mashambulio yanayoweza kutokea.

Operesheni hii inaongozwa na makamanda wawili wenye uzoefu nchini, wataalamu wawili wa vita vya msituni. Chaguo ambalo linatoa ishara kwamba nchi nzima imegeuka kuwa eneo la mzozo.

Kupelekwa kwa jeshi kunaongeza hali kuwa tete baada ya siku ya Jumanne serikali kuagiza kufungwa kwa mitandao yote ya kijamii, hususan Facebook, Twitter na WhatsApp, inayotuhumiwa kuingilia mjadala wa umma.

Matokeo ya uchaguzi yanatarajiwa kutangazwa ndani ya kipindi cha saa 48 baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura, kwamujibu wa Tume ya uchaguzi nchini Uganda.