RWANDA-CORONA

Jiji Kuu la Rwanda Kigali lafungwa kutokana na janga la Corona

Jiji kuu la Rwanda, Kigali
Jiji kuu la Rwanda, Kigali RFI/Laure Broulard

Serikali ya Rwanda imetangaza makataa ya kuzuia watu kuingia au kutoka katika jiji kuu Kigali kwa muda wa majuma mawili, kutokana na kuendelea kuongezeka kwa maambukizi mapya ya virusi vya Corona, amri hiyo itaanza kutekelezwa Jumanne, Januari 19.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo imeamuliwa katika kikao cha baraza la mawaziri kilichofanyika jana Januari 18 kikiongozwa na rais wa nchi hiyo Paul Kagame kutathmini hali ya maambukizi ya virusi vya Corona na kubainika kwamba idadi ya maambukizi imeongezeka maradufu katika mji mkuu Kigali.

Kulingana na taarifa iliotolewa na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, raia wanahimizwa kupunguza mwingiliano wa kijamii na kupunguza mienendo ya kutembea isipokuwa kwa huduma muhimu.

Habari kutoka maabara ya utafti nchini Rwanda inaonesha kuwa Kigali inachukua asilimia 61 ya wagonjwa wa Covid-19 walioripotiwa nchini tangu Januari 1.

Rwanda hadi sasa imeripoti visa 11,032 vya Covid-19, kutoka jumla ya sampuli 796,867 za vipimo vya Covid-19 zilizochukuliwa tangu Machi. Jumla ya wagonjwa 142 wamefariki kutokana na virusi vya Corona.