TANZANIA-MAREKANI

Marekani yatangaza vikwazo kwa maafisa wa serikali ya Tanzania

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli. 12 Juni, 2017
Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli. 12 Juni, 2017 Ikulu/Tanzania

Marekani imetangaza vikwazo vya kuingia nchini humo maafisa wa juu wa serikali ya Tanzania, wanaotuhumiwa kuhujumu uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka uliopita na kumwezesha rais John Magufuli kushinda kwa zaidi ya asilimia 80.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo imetangazwa na Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani anayemaliza muda Wake, na kusema waliolengwa, waliharibu mchakato wa demokrasia na kukiuka haki za binadamu. Hata hivyo, majina ya maafisa hao haijawekwa wazi.

Pompeo amesema kulikuwa na vitisho vingi na kukamatwa kwa wanasiasa wa upinzani, pamoja na kuripotiwa visa vya udanganyifu katika uchaguzi huo na kuzimwa kwa mtandao, ulifanya uchaguzi huo kutokuwa huru na haki.

Hata hivyo, Tume ya uchaguzi nchini Tanzania na  Serikali kupitia waziri wake wa mambo ya nje, Palamagamba Kabudi ilieleza kwamba uchaguzi huo huru na wa haki.

Haya ni baadhi ya maamuzi ya mwisho ya utawala wa Trump, ambaye anaondolka madarakani siku ya Jumatano baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa urais uliofanyika mwaka 2020.