UGANDA-SIASA

Bobi Wine awa huru, atoa wito wa harakati za kumwondoa Museveni madarakani

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine France24

Nchini Uganda, polisi na jeshi waliondoka nyumbani kwa kiongozi wa upinzani  Bobi Wine, Jumanne  asubuhi na kuheshimu amri ya Mahakama iliyowataka kuondoka katika makaaszi hayo, wakati huu serikali ikisema itaendelea kumfuatilia.

Matangazo ya kibiashara

Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine alikuwa huru, na alikutana na viongozi waliochaguliwa kama wabunge kutoka chama chake na kuwambia waongoze njia zisizo za vurugu kumlazimisha Raisi Yoweri Museveni kuondoka ofisini haraka iwezekanavyo.

“Tunayo ushahidi mkubwa wa kutengua uchaguzi lakini tunajua Bwana Museveni ndiye aliteua majaji wa korti kuu. Korti tunayoiamini zaidi ni korti  ya umma. Nguvu za watu”

Bobi Wine alipokuwa akiongea, helikopta ya jeshi ilikuwa ikiruka  karibu na nyumba yake ikamlazimisha asimamishe hotuba kwa dakika kadhaa.

Naye rais Museveni akisherehekea miaka 35 tangu aingie madarakani kupitia vita vya ukombozi na akatoa ujumbe kwa wale wanaopinga matokeo ya uchaguzi

 “Tutashinda vurugu kwa sababu tuna uwezo. Mumeona tayari kilichotokea. Ndio maana naomba Wanainchi wote wasahau vurugu. Kwa hivyo tafadhali musikubali mipango yoyote ya kutumia vurugu au vitisho”

Badala ya hotuba yake, Robert Kyagulanyi alienda kwenye mkutano wa siri na viongozi hao hapo nyumbani kwake.

Wakati uo huo vyombo vya Usalama bado vinachunguza harakati zake hatua ambayo wanasema itamzuia kuvunja sheria.