KENYA- SIASA

Mpasuko washuhudiwa katika muungano wa NASA nchini Kenya

Viongozi wa upinzani nchini Kenya Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Raila Odinga, Moses Wetangula na Nick Salat katika mkutano jijini Nairobi January 11 2017.
Viongozi wa upinzani nchini Kenya Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Raila Odinga, Moses Wetangula na Nick Salat katika mkutano jijini Nairobi January 11 2017. REUTERS/Thomas Mukoya

Nchini Kenya, vita vya maneno kati ya vigogo wa siasa za upinzani waliounda muungano wa NASA wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2017, yanaendelea kushuhudiwa baada ya kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kusema kuwa hawezi kuwaunga mkono washirika wake wa zamani Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka kuelekea uchaguzi Mkuu mwaka 2022

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa chama chama cha ODM ambaye pia ni mbunge wa Gwassi John Mbadi, kitendo cha vigogo hao wa Nasa kukosa kusimama na kinara wa muungano huo Raila Odinga, wakati kujiapisha kama rais wa wananchi katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi, ni ishara ya uwoga, na wasitarajie Odinga kumpendekeza yeyote kuwania uongozi wa nchi.

Wanne hao, Raila Odinga, (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetangula (Ford Kenya) walibuni muungano wa NASA Januari 2017 katika jitihada za kuikabili chama tawala cha Jubilee kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huo.

Musyoka amemlaumu Odinga kwa kutumia viongozi wengine wa kisiasa kujipatia umaarufu na kisha kuwageuka kwa manufaa binafsi. Ameongeza kusema kuwa muda wa mwanasiasa huyo mkongwe umechina na sasa asitarajie kuungwa mkono kama ilivyokuwa awali.

Miezi michache baada ya kujiapisha, Odinga na Kenyatta walifanya makubaliano ya kueneza amani nchini na kuanza mchakato wa kubadilisha katiba kwa nia ya kutatua changamoto za Taifa hilo.

Wakati wa hafla hiyo, Musyoka, Mudavadi na Wetangula walidai kuzuiliwa majumbani na kupokonywa walinzi, hivyo basi kukosa kufika katika bustani ya Uhuru kwa sherehe za Raila kujiapisha kama rais wa wananchi, kitendo kilichowafanya waonekane waoga mbele ya wafuasi wao.

Watatu hao wanasemekana kutafuta dira ya kubuni muungano wao kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, huku Raila Odinga na rais Uhuru Kenyatta wakiendelea kuipigia debe mchakato wa maridhiano (BBI) kwa madai ya kuunganisha Taifa kwa utawala bora.