Uchina-Urusi

Uchina na Urusi kuendelea kushinikiza utumizi wa mazungumzo katika mzozo wa Syria

Uchina na Urusi zinaahidi kuongeza ushirikiano wao katika Umoja wa Mataifa ili kutafuta suluhu la machafuko yanayoendelea nchini Syria.Rais wa Uchina Hu Jintao na mwenyeji wake, rais wa Urusi Vladimir Putin wote wamesisitiza kuwa machafuko hayo yanaweza kutatuliwa tu kwa njia ya amani.

Matangazo ya kibiashara

Aidha, marais hao wameongeza kuwa wanatarajia rais Bashar Al Assad ataondoka madarakani kwa njia ya amani na kuonya kuwa hazitaunga mkono juhudi zozote za utumizi wa majeshi dhidi ya uongozi wa Damascus.

Urusi na Uchina kwa muda mrefu zimekuwa zikitumia kura zao za veto kupinga kupitishwa kwa azimio lolote dhidi ya uongozi wa rais Assad, na kusisistiza kuwa machafuko nchini humo yanaweza kutatuliwa tu na raia wenyewe wa Syria kwa njia ya mazungumzo.

Marekani na mataifa mengine ya Ulaya kwa upande wao yameendelea kuilaumu Moscow na Beijing kuhusu sera yao kuhusu machafuko ya Syria,ikisema Moscow na Beijing zinachangia kuogezeka kwa machafuko hayo.

Siku ya Jumatatu,viongozi wa Umoja wa Ulaya walikutana na rais Putin na kumtaka kuuungana na mataifa mengine ya Ulaya kumaliza machafuko yanayoendelea Syria kwa kuhakikisha kuwa mpango wa amani uliopendekezwa na msuluhishi wa kimataifa wa mgogoro huo Koffi Annan unazingatiwa.

Zaidi ya watu elfu 13 wameuawa tangu machafuko dhidi ya rais Assad yalipoanza miezi 15 iliyopita.