SYRIA-MAREKANI

Marekani yataka Syria kuwekewa vikwazo zaidi vya kiuchumi

Marekani imeunga mkono pendekezo la Muungano wa nchi za Kiarabu kupitisha azimio la kuiwekea vikwazo zaidi vya kiuchumi serikali ya Syria kutokana na machafuko yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo, Marekani haijaweka wazi ikiwa pia inaunga mkono kupitishwa kwa azimio la kutaka Umoja wa Mataifa kutuma majeshi yake nchini Syria kumwondoa rais Bashar Al Assad madarakani kama ilivyoshuhudiwa nchini Libya.

Timoth Geithner Waziri wa fedha  wa Marekani  amesema kuwa mataifa mengine yanayopinga machafuko nchini Syria yana jukumu la kuhakikisha kuwa, wanaunga mkono Washinton DC katika harakati zake za kumaliza mauji dhidi ya raia nchini Syria.

Waziri wa nchi za kigeni wa Marekani Hillary Clinton anaongoza mawaziri wengine wa nchi za kigeni kutoka Uingereza, Ufaransa na Uturuki pamoja na mataifa mengi kutoka Jumuiya ya Kiarabu kuzungumzia hatima ya Syria.

Mawaziri hao wanazungumzia namna ya utekelezwaji wa mpango wa amani wa Koffi Annan ambaye ni msuluhishi mkuu wa mgogoro huo ambao umeonekana kutozaaa matunda yeyote ya kumaliza machafuko hayo .

Wakati uo huo rais Bashar Al Assad,amemteua Riyad Hijab kama Waziri Mkuu kuunda serikali mpya.

Hijab ni waziri wa zamani Kilimo nchini na amepata wadhifa huo baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa wabunge mapema mwezi uliopita.