UN

LRA yawasajili watoto 600 katika jeshi lake-UN

Umoja wa Mataifa unasema kundi la waasi la Lords Resistance Army (LRA) linaloongozwa na Josph Kony raia wa Uganda limewateka nyara watoto zaidi ya 600 na kuwalazimisha kujiunga na kundi hilo kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita .

Matangazo ya kibiashara

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa kundi hilo la LRA ambalo chimbuko lake ni Kasakazini mwa Uganda, limewateka watoto hao katika mataifa ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini, na watoto hao wanatumiwa kama watumwa wa kimapenzi katika kundi hilo.

Mbali na hayo,  watoto 45 wameuliwa na kundi hilo kati ya Julai mwaka 2009 na Februari mwaka huu wa 2012, huku ripoti hiyo ikiongeza kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka zaidi katika siku zijazo.

Mbali na kutumiwa kama watumwa wa kimapenzi katika kundi hilo, watoto hao hutumiwa kuwauawa ndugu zao wakiwemo wazazi wao baada ya kulazimishwa kuingia katika kundi hilo .

Kundi la LRA lililoanzishwa miaka 20 iliyopita Kaskazini mwa Uganda kwa sasa linakadiriwa kuwa na kati ya wanajeshi 300 na 500 nusu yao wakiwa ni watoto .

Majeshi ya Uganda yakishirikiana na yale ya Umoja wa Afrika na wanajeshi 100 kutoka Marekani wanaendeleza msako wa kumtafuta Joseph Kony ambaye anashukiwa kujificha katika misitu ya Jamhuri ya Afrika ya Kati,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini.

Kony anatafutwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya ICC kwa kutekeleza mauji ya malefu ya watu na kusabisha visa vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu.