SYRIA

Koffi Annan asema mpango wa amani nchini Syria hautekelezwi

Msuluhishi wa kimataifa kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Syria Koffi Annan ameonya kuwa Syria inaelekea katika vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiwa juhudi za haraka hazitachukuliwa .

Matangazo ya kibiashara

Annan aidha, amekiri kuwa mpango wake wa amani ulionuiwa kumaliza machafuko hayo hauzingatiwi na serikali ya Syria pamoja na baraza la upinzani nchini humo, na wakati umefika wa Jumuiya ya Kimatifa kuchukua hatua nyingine.

Msuluhishi huyo ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani kuwa wakati wa Jumuiya ya Kimataifa kuzungumza kwa sauti moja ni sasa na hilo linaloweza kuwa suluhu la machafuko nchini Syria, nchi ambayo maelfu ya watu wameuawa tangu machafuko hayo yalipoanza kushuhudiwa miezi 15 iliyopita.

Annan alikuwa anazungumza na wajumbe wa Baraza la Usalama wa Umoja wa mataifa siku moja tu baada ya mauji ya watu 55 katika mji wa Hama, mauji ambayo yameshtumiwa kimataifa.

Serikali ya Syria inatuhumiwa kuyahami makundi ya kigaidi kuvamia ngome za upinzani na kutekeleza mauji hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton ametaka rais Bashar Al Assad kuacha madaraka mara moja na kuondoka nchini humo kwa kile Clinton anasema rais Assad ameendelea kuwaua raia wake.

Waangalizi wa Umoja wa Mataifa wanasema wamezuiliwa kufika katika mji wa Hama kujionea miili ya watu waliuawa na kuthmini namna mauji hayo yalivyofanyika kitendo ambacho Koffi Annan amesema kinatishia usalama wa waangalizi hao.