BULGARIA-ISRAEL

Bulgaria yatoa kanda ya mshukiwa wa shambulizi la bomu

Serikali ya Bulgaria imetoa kanda ya Video ikimwonesha mshukiwa aliyesababisha shambulizi la bomu katika basi lililokuwa limewabeba watalii wa Israeli. 

Matangazo ya kibiashara

Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu saba wakiwemo raia watano wa Israeli na kuwajeruhi wengine zaidi ya 30 shambulizi  linaloshukiwa kupangwa na Iran.

Kanda hiyo ya Video inamwonesha mshukiwa huyo aliyekuwa kama mtalii akizururazura na mfuko kabla ya watalii hao kuingia ndani ya basi la kuwasafirisha kutoka katika uwanja wa ndege.

Bulgaria inasema mshukiwa huyo alikuwa na vitambulisho vya Marekani na  rais  Barrack Obama amelaani shambulizi hilo ambalo ni baya zaidi kuwahi kutekelezwa dhidi ya raia wa Israeli ugenini.

Waziri Mkuu wa Isreali Benjamin Netanyahu amesema serikali yake itatumia nguvu dhidi ya Iran kwa kutekeleza shambulizi hilo ambalo  Tehran imekanusha kuhusika.

Naye Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak amesema hakuna ubishi wa aina yoyote kwamba shambulizi hilo ni la kigaidi na lilitekelezwa na Iran na linafanana na mashmabulizi  ya awali yaliyowalenga raia wa Israel ugenini kama ilivyoshudiwa katika miaka ya awali nchini Kenya,India,Thailand, Azerbaijan, na  Cyprus .