CHINA-AFRIKA

China yaahidi Dola Bilioni 20 kwa bara la Afrika

China imetangaza kutoa mkopo wa Dola Bilioni 20 kwa mataifa ya Afrika kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo kuyasaidia mataifa ya bara hilo kuinua uchumi wake na kuendeleza mipango ya maendeleo.

Matangazo ya kibiashara

Rais Hu Jintao ametoa ahadi hiyo jijini  Beijing katika mkutano wa kimataifa kati ya China na zaidi ya viongozi 50 kutoka barani Afrika, kujadili uhusiano wa kibiashara kati ya bara hilo na China.

Jintao amesema fedha hizo zitatumiwa kukarabati miundombinu na kuanzisha miradi ya biashara ndogo ndogo miongoni mwa wafanyibiashara barani Afrika.

Beijing pia imeahidi kutoa msaada wa mafunzo kwa wataalam mbalimbali barani Afrika wakiwemo wanafunzi kwa kuwalipia karo chini ya muungano wa  Umoja wa Afrika.

Kwa miaka 15, iliyopita serikali ya China imekuwa ikishirikiana kwa karibu sana na mataifa ya Afrika na kuwekeza zaidi na hata kupewa kandarasi za kujenga barabara na majengo.

Ushirikiano wa kibiashara  kati ya China na Afrika mwaka uliopita ulifikia dola Bilioni 166 nukta 3 ikilinganishwa na dola Bilioni 20 miaka kumi zilizopita.