SYRIA

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupigia kura azimio dhidi ya Syria

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kupigia kura azimio dhidi ya serikali ya Syria inayoongozwa na rais Bashar Al Assad siku moja baada ya shambulizi la bomu jijini Damascus kusababisha kifo cha waziri wa Ulinzi Daoud Rajha na shemeji wa rais Assad Assef Shawkat. 

Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na msuluhishi wa mzozo huo Koffi Annan wametaka wajumbe wa baraza hilo  kuhakikisha kuwa wanachukua hatua nzito dhidi ya uongozi wa rais Bashar Al Assad.

Hata hivyo, Urusi na Uchina zinatarajiwa kutumia kura zao za veto kupinga azimio lolote dhidi ya  serikali ya Syria kwa kile mataifa hayo yanaamini kuwa suluhu la Syria liko mikokoni mwa raia wenyewe wala sio mataifa ya kigeni.

Kiongozi wa waangalizi nchini humo Jenerali Robert Mood amesema haoni nchi hiyo ikielekea katika njia ya amani kutokana na ongezeko la mapigano wakati  majeshi ya serikali yakitoa saa 48 kwa wakaazi wa mji huo kuondoka katika maeneo ambayo makabiliano kati yao na wapiganaji wa upinzani yanaendelea.

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Syria wanasema kuwa zaidi ya watu 200 walipoteza maisha yao siku ya Jumatano iliyopita ikiwemo watu 38 mjini Damascus.

Machafuko nchini Syria yamekuwa yakiendelea kwa kipindi cha miezi kumi na sita na kusabaisha maelfu ya watu kuuawa.