SYRIA

Mkuu wa kitengo cha usalama nchini Syria afariki wakati mapigano yakiendelea Damascus

Kiongozi wa kitengo cha kitaifa cha usalama nchini Syria Hisham Ikhtiar amefariki kutokana na majeraha aliyoyapata wakati wa shambulizi la kujitoa mhanga jijini Damascus wiki hii na kusababisha kifo cha waziri wa Ulinzi.

Matangazo ya kibiashara

Mapigano makali yameendelea kushuhudiwa jijini Damascus kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa upinzani huku, balozi wa Urusi nchini Ufaransa Alexander Orlov akisema rais Bashar Al Assad yuko tayari kujiuzulu.

Orlov anadai Assad alikubali kuachia ngazi wakati wa mkutano kati ya wajumbe wa serikali ya Syria na upinzani mwezi uliopita mjini Geneva nchini Swizerland madai ambayo Syria inasema si ya kweli.

Waasi nchini Syria wamefanikiwa kuchukua uthibiti wa maeneo ya vituo vya mpakani baina ya nchi hiyo na jirani zao wa Uturuki na Iraq na kusimika bendera zao kudhihirisha utawala wao katika eneo hilo.

Maeneo hayo yanatekwa na waasi hao baada ya  Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN kutofautiana juu ya msimamo wao wa kuiweka vikwazo serikali ya Bashar Al Assad .

Mataifa ya Magharibi yameendelea kukerwa na kitendo cha China na Urusi kupinga kuunga mkono azimio la kuiwekea vikwazo nchi ya Syria katika harakati za kujaribu kumaliza machafuko hayo .

Msuluhishi wa kimataifa wa mzozo huo Koffi Annan kabla ya kikao cha wajumbe wa baraza hilo alitaka baraza hilo kuchukua hatua kali dhidi ya serikali ya Syria kutokana na kuendelea kwa machafuko nchini humo.

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, wajumbe wa Umoja huo wanatajadili uwekezekano wa kuwaongezea muda waangalizi wa kijeshi nchini Syria,kutokana na muda wao kukamiliki Ijumaa hii.

Umoja wa mataifa ulituma wanajeshi wake 300 nchini Syria miezi mitatu iliyopita kuchunguza utekelezaji wa mpango wa Koffi Annan wa kumaliza machafuko hayo lakini wakasitisha shughuli zao mwezi wa Juni kutokana na kuendelea kwa machafuko nchini humo.

Uingereza inapendekeza kuwaongezea muda wa mwezi mmoja waangalizi hao wa Umoja wa Mataifa  nchini Syria.