SYRIA

Waziri Mkuu wa zamani wa Syria Riad Hijab asema uongozi wa rais Assad unaporomoka

Waziri Mkuu wa zamani wa Syria Riad Hijab aliyejionndoa katika serikali ya rais Bashar Al Assad wiki iliyopita, amesema uongozi wa rais Assad unaanguka. 

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza akiwa mjini Amman nchini Jordan, Hijab amesema uongozi wa Assad unaporomoko kifedha, kimaandili na kijeshi na kwa sasa majeshi yake hayathibiti zaidi ya asilimia 30 ya taifa hilo.

Aidha, Hijab ameutaka upinzani kusimama pamoja na  kuhimiza wanajeshi wa Syria kuungana na upande wa mapambano ambao amesema unaungwa mkono na idadi kubwa ya watu wa Syria.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani kuzungumza na hadharani tangu alipojiodnoa katika serikali ya rais Assad siku kadhaa zilizopita wakati huu mapigano yakiendelea kushuhudiwa kati ya waasi na wanajeshi wa serikali katika mji wa Allepo.

Katika hatua nyingine, uongozi wa rais Bashar Al Assad unaendelea kupata shinikizo zaidi za kuondoka madarakani baada ya muungano wa mataifa 57 ya kiislamu kutaka Syria kuondolewa katika muungano huo.

Mshirika wa karibu wa rais Bashar Al Assad Bouthaina Shaaban, yuko nchini China kushauriana na waziri wa mambo wa nje wa nchi hiyo Yang Jiechi kuhusu mzozo unaoendelea katika nchi yake.

China ambayo imekuwa ikishirikiana na Urusi kupinga azimio lolote dhidi ya serikali ya Syria, imeendelea kusisitiza kuwa suluhu la Syria lipo mikononi mwa watu wa Syria wenyewe na wanaunga mkono mapendekezo sita ya aliyekuwa mpatanishi wa kimataifa wa mzozo huo Koffi Annan aliyejiuzulu.

Mkurungenzi Mkuu wa maswala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Valerie Amos amewasili nchini Syria kuthathmini hali ya kibindamu nchini humo wakati huu ambapo maelfu ya wakazi wa miji mbalimbali wamekimbilia mataifa jirani.

Mzozo wa Syria umedumu kwa miezi 17 sasa na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha yao, huku suluhu la mzozo huo likiwa bado halijapatikana jambo ambalo Propfesa Larry Gumbe mchambuzi wa siasa za kimataifa kutoka Nairobi nchini Kenya anasema jumuiya ya kimatraifa imeshindwa kutatua mzozo huo.