AFGANISTAN

Mashambulizi nchini Afganistan yaua zaidi ya watu 30

Kundi la walipuaji wa bomu wa kujitoa mhanga wamejilipua katika maeneo mbalimbali katika mji wa Zaranj nchini Afganstan na kusababisha kuuawa kwa zaidi ya watu thelatini na kuwajeruhi wengine zaidi ya mia moja.

Matangazo ya kibiashara

Maafisa wa usalama nchini humo wanasema hayo ndiyo mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika mji huo katika siku za hivi karibuni ulioko katika mpaka wake na Iran.

Maeneo yenye watu wengi kama masoko ndiyo yaliyolengwa, wakati mamia ya watu wakifanya ununuzi wa bidhaa za sherehe za Idd itakayoadhimishwa wiki ijayo.

Maafisa wa usalama nchini Afganistan wanaonya kuwa huenda mashambulizi zaidi yakashuhudiwa nchini humo.

Maelfu ya watu wameuauwa nchini Afganistan mikononi mwa kundi la Taliban tangu majeshi ya Kimataifa yalipokwenda nchini humo mwaka 2001 kulinda amani na kupambana na makundi ya kigaidi.

Majeshi ya NATO nchini Afganistan yanatarajiwa kuondoka nchini humo kufikia mwaka 2014.