SYRIA

Mauji zaidi yaripotiwa mjini Allepo nchini Syria

Ndege za kivita za Syria zimeshambulia makaazi ya watu katika eneo la Azaz mjini Allepo  na kusababisha kuuawa kwa zaidi ya watu thelathini wakiwemo watoto,huku mashirika ya kutetetea haki za binadamu nchini humo yakisema maelfu ya watu wanakimbilia nchini Uturuki .

Matangazo ya kibiashara

Mkurugenzi Mkuu wa maswala ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Valerie Amos, ambaye anazuru nchi hiyo amesema watu Milioni 2 nukta 5 wanahitaji msaada wa kibinadamu ikiwemo makaazi,chakula na matibabu.

Kwingineko, Syria imesimamishwa kama mwanachama wa Muungano wa nchi za Kiislamu OIC, kutokana na machafuko yanayoendelea nchini hum

Wajumbe kutoka mataifa hayo 57 wa muungano wa nchi hizo wamekuwa wakikutana mjini Mecca nchini Saudi Arabia kwa siku mbili zilizopita kujadili hatima ya Syria kama mwanachama wake.

Wajumbe katika mkutano huo wameafikia kwa kauli moja kuindoa Syria kama mwanachama wake  kwa kile walichokisema kuwa ni kutokana na machafuko wanayosema yanachangiwa na serikali ya rais Bashar Al Assad, na kusababisha maelfu ya watu kuuawa na kutoroka makwao.

Kiongozi wa Muungano huo Ekmeleddin Ihsanoglu amesema mataifa ya Kiislamu yanaunga mkono kumalizika kwa machafuko nchini Syria na suluhu kupatikana kwa njia ya amani na inaungana na mataifa mengine duniani yanayotaka machafuko kukamilika nchini Syria.

Marekani kupitia kwa msemaji wa mambo ya nje Victoria Nuland amesema hatua hiyo ya mataifa ya Kiislamu yametuma ujumbe mzito kwa serikali ya Damascus ambayo amesema imeendelea kutengwa kimataifa.