NATO-UTURUKI-SYRIA-MAREKANI

Clinton: NATO inahitaji pongezi, waidhinisha ombi la Uturuki kulinda mipaka yake

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton (kushoto) akisalimiana na katibu mkuu wa majeshi ya NATO, Anders Fogh Rasmussen
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton (kushoto) akisalimiana na katibu mkuu wa majeshi ya NATO, Anders Fogh Rasmussen Reuters

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton amepongeza jumuiya ya majeshi ya nchi za kujihami za magharibi NATO kwa hatua ambayo imepiga mpaka sasa katika kuzilinda nchi wanachama. 

Matangazo ya kibiashara

Waziri Clinton ameyasema hayo wakati wa mkutano wa siku mbili wa nchi wanachama za NATO waliokuwa wanakutana mjini Brussels kujadili ombi la nchi ya Uturuki kutaka kupatiwa msaada wa kijeshi toka jumuiya hiyo.

Clinton ambaye hii inakuwa ziara yake ya mwisho kama waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani kufuatia kumaliza muda wake, amesema kuwa NATO inabidi kupongezwa kwa mafanikio ambayo imeyapata mpaka sasa, ikiwemo vita kule nchini Afghanistan na ile ya Libya.

Siku ya Jumatano nchi wanachama za NATO zilikubaliana kwa kauli moja kuiidhinishia mitambo maalumu ya kulipua maroketi nchi ya Uturuki kwaajili ya kulinda mipaka yake.

Uturuki iliwasilisha ombi maalumu kwenye jumuiya hiyo ikidai kuwa siku za hivi karibuni kumekuwa kukirushwa maroketi toka upande wa nchi ya Syria na kutua kwenye ardhi yake jambo ambalo ni hatari kwa usalama na inabidi nchi hiyo kujilinda.