MAREKANI

Rais Barack Obama aapishwa Ikulu kuongoza kwa awamu ya pili

Rais Barack Obama akila kiapo Ikulu siku ya Jumapili
Rais Barack Obama akila kiapo Ikulu siku ya Jumapili Reuters

Rais wa Marekani, Barack Obama amepishwa rasmi siku ya Jumapili kushika nafasi hiyo kwa awamu ya pili katika sherehe ambazo zilifanyika kwa siri kwenye ikulu ya nchi hiyo. 

Matangazo ya kibiashara

Jaji mkuu John Roberts ndie aliyesimamia zoezi la kuapishwa kwa rais Obama wakiwa kwenye chuma maalumu cha Ikulu, sherehe ambazo zilishuhudiwa na familia yake pamoja na makamu wake wa rais Joe Biden.

Kuapishwa kwa rais Obama siku ya Jumapili kulitokana na matakwa ya katiba ya nchi hiyo ambayo inataka rais kuapishwa tarehe 20 ya mwezi January na kwakuwa siku hiyo iliangukia siku ya Jumapili walilazimika kutekeleza matakwa ya katiba.

Sherehe rasmi za kuapishwa kwa kiongozi huyo zinatarajiwa kufanyika kwenye mji wa US Capitol ambapo maelfu ya wananchi wa taifa hilo wanatarajiwa kushuhudia rais Barack Obama akirudia tena kiapo chake alichotekeleza siku ya Jumapili.

Sherehe hizo zinafanyika wakati ambapo pia ni maadhimisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwa mwanaharakati wa haki za watu weusi Martin Luther King jambo ambalo linafanya sherehe hizo kuwa maalumu zaidi na zakipekee.

Mara baada ya kuapishwa hapo jana rais Obama hakusema neno lolote badala yake anatarajiwa kufanya hivyo hii leo mbele ya maelfu ya wananchi ambao watakuwa wakishuhudia tukio la kuapishwa kwake.