MALI-ECOWAS-UFARANSA

Jeshi la Mali kuwachunguza wanajeshi wake kufuatia tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu

Jenerali  Ibrahima Dahirou wa jeshi la Mali akizungumza mjini Bamako
Jenerali Ibrahima Dahirou wa jeshi la Mali akizungumza mjini Bamako AFP/ ISSOUF SANOGO

Kundi moja la waasi wa kiislamu nchini Mali linaloshikilia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo limetangaza kutaka kuwa na mazungumzo na viongozi wa Serikali kujaribu kutafuta suluhu kwenye eneo la kaskazini. 

Matangazo ya kibiashara

Kundi la Ansar al-Dine ambalo sasa limegawanyika limesema kuwa linataka kufanya mazungumzo na Serikali ili kunusuru vifo zaidi ambavyo vinatokana na mapigano yanayoendelea kaskazini mwa nchi hiyo kwenye operesheni inayoongozwa na vikosi vya Ufaransa.

Hapo jana baadhi ya viongozi wa kundi hilo ambao wamejitenga na wenzao wamesema wako tayari kujiunga upande wa Serikali katika kukabiliana na makundi mengine ya kiislamu kama yale ya MNLA na Tuareg abayo yamesema harakati zao zinatambulika toka awali.

Kujitenga kwa kundi hilo kumepokelewa kwa hisia tofauti na wachambuzi wa masuala ya siasa ambao wanaona kuwa iweje kundi hilo lijitenge sasa wakati huu ambapo mashambulizi ya kuwasambaratisha yamechacha na wanakaribia kushindwa.

Hata hivyo Serikali ya Mali imetupilia mbali madai ya kundi hilo na kuongeza kuwa vita hivyo vitaendelea mpaka pale watakapohakikisha wamewasambaratisha na kuleta amani kwenye maeneo hayo.

Katika hatua nyingine Serikali ya Mali imetangaza kuanzisha uchunguzi dhidi ya wanajeshi wake wanaodaiwa kushiriki vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu kwenye operesheni ianyoendelea kuelekea kaskazini mwa nchi hiyo.

Msemaji wa jeshi la Mali Luteni Kanali Diarra Nkone amethibitisha kuanza kwa uchunguzi huo ambao amedai unalenga kubaini iwapo kumekuwa na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu kunakofanywa na wanajeshi wa Mali.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo yameripoti kuwa wanajeshi wa Mali wamekuwa wakiwaua mateka wa kiislamu ambao wamekuwa wakiwakamata pamoja na kupora mali kwenye baadhi ya miji ambayo ilikuwa inakaliwa na waasi hao.