VATICAN

Papa Benedicto wa 16 kujiuzulu wadhifa wake tarehe 28 mwezi huu

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Benedicto wa 16 ametangaza atajiuzulu kufikia mwisho wa mwezi huu wa pili.

Matangazo ya kibiashara

Kujiuzulu kwa kiongozi huyo kumetokea ghafla na kuwashangaza waumini wa Kanisa hilo duniani,huku Papa akisema amefikia uamuzi huo kwa sababu ya umri wake mkubwa.

Papa Benedicto mwenye umri wa miaka 85 amesema hawezi tena kuhudumu kama kiongozi wa Kanisa hilo ambalo amekuwa akiongoza tangu mwaka 2005 baada ya kufariki kwa Papa John Paul wa pili.

Kujiuzulu kwa kiongozi wa juu wa Kanisa Katoliki duniani ni jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Kanisa hilo na hii ndio mara ya kwanza, huku viongozi watano waliopita wakifia madarakani.

Haijabainika wazi ni nini ambacho kiongozi huyo atajihusisha nacho baada ya kujiuzulu tarehe 28 mwezi huu.

Papa ambaye jina lake halisi ni Joseph Ratzinger kutoka Ujerumani alichukua uongozi wa Kanisa hilo wakati likikumbwa na kashfa za viongozi wa kanisa hilo kuwadhalalisha watoto kimapenzi.

Msemaji wa Vatican ambako ndiko makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani Federico Lombardi amesema kuwa kiongozi mpya wa kanisa hilo atachaguliwa mwezi ujao.

Papa mpya huchaguliwa na kundi la Makadinali kutoka kote duniani ambao hukutana mjini Vatican kufanya uchaguzi huo.