KOREA KASKAZINI

Mataifa yenye nguvu duniani yalaani Korea Kaskazini

Mataifa yenye nguvuĀ  duniani yamelaani hatua ya Korea Kaskazini kujaribu zana zake za Nyuklia licha ya onyo la kutofanya hivyo kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa mataifa hayo ni pamoja na Marekani,China na Urusi ambayo kwa pamoja viongozi wake wameungana kukashifu hatua hiyo ya Pyongyang, na kutaka ichukuliwe hatua ya kuwekewa vikwazo zaidi.

Korea Kaskazini inasema imefanikiwa kufanya jaribio la ardhini la zana zake za Nyuklia na kuzua shutuma nzito kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Serikali ya Pyongyang inasema jaribio hilo la tatu limefanikiwa pakubwa sana na limefanyika kwa utalaam wa hali ya juu.

Rais wa Marekani Barrack Obama ameshtumu hatua hiyo ya Korea Kaskazini na kusema kuwa ni sharti Jumuiya ya Kimataifa ichukue hatua dhidi ya serikali hiyo kwa kile alichokieleza hatua hiyo inatishia usalama wa Marekani na wa dunia nzima.

Awali,Ā  Umoja wa Mataifa ulikuwa umeonya serikali ya Pyongyang kuwa itachukuliwa hatua ikiwa itafanya jaribio lingine la zana zake za Nyuklia.

Tayari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ameshtumu hatua hiyo anayosema imevunja azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kufanya jaribio hilo.

Wajumbe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanakutana siku ya Jumanne kujadili hatua hiyo ya Pyongyang na kuona ni hatua gani watakayochukua dhidi ya serikali hiyo.

Korea Kaskazini awali ilifanya majaribio ya zana zake mwaka 2006, 2009 na mwezi Januari ilitangaza kuwa itafanya majaribio yake wakati wowote licha ya onyo kutoka kwa Umoja wa Mataifa.

Jaribio la Korea Kaskazini limezua hali ya wasiwasi katika mataifa jirani kama Japan na Korea Kusini huku viongozi wanaohusika na usalama wakikutana kujadili tahadhari inayoweza kuchukua.