Marekani

Mazungumzo ya Kimataifa kuhusu silaha yaanza New York Marekani

Mabalozi kutoka kote  duniani wameanza mkutano katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani kujadili kuhusu uuzwaji na ununuzi wa silaha.

Matangazo ya kibiashara

Lengo la mkutano huo ni kuzuia uuzwaji wa silaha haramu baada ya mazunguzo kama hayo kutozaa matunda mwezi Julai mwaka uliopita kutokana na mataifa makuu kama Marekani, China na Urusi kutofautiana kuhusu mkataba huo.

Mazungumzo hayo yatadumu kwa kipindi cha wiki mbili zijazo huku Marekani kupitia Waziri wa mambo ya nje John Kerry akisema taifa lake linatarajiwa kupata suluhu na mataifa mengine.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema mkataba wa pamoja utasaidia kupunguza mauaji kupitia silaha katika mataifa yanayokumbwa na machafuko.

Wito wa Ban Ki Moon ameungwa mkono na Mashirika ya Kimataifa ya kutetea haki za binadamu kama Amnesty International ambalo pia limetaka suluhu kupatikana ili kuepuka ukiukwaji wa haki za binadamu kutumia silaha ndogondogo.

Mataifa ya Syria, Mali na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni baadhi ya nchi ambazo silaha ndogondogo zimekuwa zikitumiwa kutekeleza mauji.