ZAMBIA

Rais wa zamani wa Zambia, Rupiah Banda akamatwa na kuachiwa kwa dhamana, kupanda kizimbani Jumanne

Rupiah Banda, rais wa zamani wa Zambia anayeshtakiwa kwa tuhuma za rushwa wakati akiwa rais
Rupiah Banda, rais wa zamani wa Zambia anayeshtakiwa kwa tuhuma za rushwa wakati akiwa rais Reuters

Mamlaka nchini Zambia zimemkamata na kumfikisha mahakamani aliyekuwa rais wa taifa hilo Rupiah Banda, hatua inayokuja ikiwa yamepita majuma kadhaa toka bunge la nchi hiyo limuondolee kinga ya kutoshtakiwa. 

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa msemaji wa jopo la wapelelezi waliokuwa wakimchunguza kiongozi hiyo amethibitisha kukamatwa kwa Banda na kapandishwa kizimbani kujibu mashtaka yanayomkabili ya matumizi mabaya ya ofisi.

Juma moja lililopita wachunguzi wa kesi ya banda waliahirisha zaidi ya mara mbili kumuhoji kiongozi huyo hadi leo alipotoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi huyo ambaye sasa yuko nje kwa dhamana baada ya mahakama kukubali ombi la upande wa utetezi kutaka mteja wao apatiwe dhamana.

Kiongozi huyo anatarajiwa kupandishwa kizimbani tena siku ya Jumanne kuanza kusikiliza rasmi mashtaka zaidi ambayo yanamkabili.

Serikali ya rais Michael Satta inamtuhumu Banda na waliokuwa mawaziri wake kushiriki vitendo vya rushwa hasa katika utiwaji wa saini wa mkataba wa mafuta na kampuni moja ya mafuta toka nchini Nigeria.

Mawakili wa utetezi wamesema kuwa hatua ya Banda kufunguliwa kesi ni mpango wa rais Satta na utawala wake unaolenga kugandamiza upinzani nchini humo usiwe na sauti.

Banda mwenyewe amekanusha kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa utawala wake na kuongeza kuwa yote aliyoyafanya yalikuwa ni kwamanufaa ya wananchi wa Zambia.