SYRIA-UTURUKI-MAREKANI

Taarifa mpya zaibuka kuhusu nchi za Kiarabu kuwasaidia kwa silaha waasi wa Syria

Wapiganaji wa Syria wakiwa kwenye mji wa Idlib wakiendelea na makabiliano dhidi ya vikosi vya Serikali
Wapiganaji wa Syria wakiwa kwenye mji wa Idlib wakiendelea na makabiliano dhidi ya vikosi vya Serikali REUTERS/Mohamed Kaddoor

Nchi za Kiarabu, Uturuki kwa kushirikiana na shirika la ujasusi la Marekani CIA zimeongeza nguvu zaidi za kuwasaidia kwa silaha waasi wa Syria wanaopigana na serikali ya Syria. 

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa taarifa za siri zilizochapishwa kwenye gazeti la the New York Times la nchini Marekani, limeeleza kwa kina mpango uliopo kati ya nchi za Kiarabu, Uturuki na Marekani ambao sasa wanashirikiana kuwasadia kwa silaha waasi.

Taarifa hizo za siri zinatolewa wakati ambapo Jumuiaya ya Kimataifa bado haijaiondolewa vikwazo vya kuuziwa silaha waasi wa Syria kwakile wanachohofia silaha hizo kufika kwenye mikono ya watu wasio salama.

Hata hivyo Serikali zote hazijakubali wala kukataa kushirikiana katika kuwapatia silaha waasi wa Syria ambao wanaendelea a makabiliano makali na wanajeshi watiifu wa rais Bashar al-Asad.

Taarifa hizo zinatolewa wakati ambapo mkuu wa Upinzani, Ahmed Moaz al-Khatib ametangaza kujiuzulu nafasi yake kama kiongozi wa muungano wa upinzani kwa kile alichoeleza kutoridhishwa na jinsi jumuiya ya kimataifa inavyoshughulikia mzozo wa Syria.

Tangazo la kujiuzulu kwa Moaz alilitoa kwenye mtandao wake wa kijamii wa facebook ambapo amesema kuwa amelazimika kufanya hivyo kutokana na Jumuiaya ya kimataifa kushindwa kushughulikia ipasavyo mzozo wa Syria.

Tangazo la kiongozi huyo limekataliwa na wajumbe wa Baraza la mpito la Syria ambalo limesisitiza kuutambua mchango wake na kumsisitiza kutoachia madaraka yake kama kiongozi wao.

Moaz ameongeza kuwa anaachia madaraka yake ili afanye kazi kwa uhuru zaidi kwa kile alichodai anapigania uhuru wa Syria kupitia taasisi ambayo inashindwa kutekeleza majukumu yake kwa umoja.