Watu saba wauawa kwenye mapigano mapya kwenye mji wa Gao nchini Mali
Watu saba wameripotiwa kupoteza maisha akiwemo mwanajeshi mmoja wa vikosi vya Mali kufuatia mapigano yaliyozuka siku ya Jumapili kaskazini mwa nchi hiyo kwenye mji wa Gao kati yao na waasi wa kiislamu waliokuwa wametwaa maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Waasi hao wa kiislamu ambao wanauhusiano wa karibu na mtandao wa kigaidi duniani wa Al-Qaeda wametishia kuwaua mateka waote raia wa Ufaransa ambao inawashikilia kufuatia uvamizi wa majeshi ya Ufaransa nchini Mali.
Mapigano hayo yalizuka wakati wanajeshi wa Mali walikuwa wakiendesha operesheni maalumu ya kuusafisha mji huo baada ya kudaiwa kuwa baadhi ya wapiganaji wa kiislamu wamerejea kwa siri kwenye mji wa Gao.
Msemaji wa vikosi vya Mali vilivyoshiriki operesheni hiyo, amethibitisha kujeruhiwa kwa wanajeshi wake kikiwemo kifo cha mwanajeshi mmoja huku wengine waliouawa wanadaiwa kuwa ni wapiganaji wa kundi la MUJAO.
Wapiganaji hao wameongeza shinikizo kwa familia ambazo ndugu zao wanashikiliwa mateka wakilenga kuishinikiza serikali ya Ufaransa kuachana na operesheni yake inayoendelea kuitekeleza nchini humo.
Juma lililopita kundi hilo lilitangaza kumuua raia wa sita wa Ufaransa kati ya inaowashikilia, tangazo ambalo mpaka sasa Serikali ya nchi hiyo bado haijathibitisha.