AFRIKA KUSINI-NIGERIA

Henry Okah ahukumiwa kifungo cha miaka 24 jela na mahakama nchini Afrika Kusini kwa makosa ya ugaidi

Henry Okah akitoka kwenye mahakama ya Afrika Kusini baada ya kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 24 jela
Henry Okah akitoka kwenye mahakama ya Afrika Kusini baada ya kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 24 jela Reuters

Mahakama moja nchini Afrika Kusini imemuhukumu kifungo cha miaka ishirini na nne jela, Henry Okah raia wa Nigeria anayetuhumiwa kushiriki vitendo vya kigaidi ikiwemo tukio la mabomu mjini Abuja mwaka 2010.

Matangazo ya kibiashara

Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi dhidi ya Okah, jaji Neels Claassen amesema kuwa mahakama yake imejiridhisha pasipo na shaka kuwa Okaha alipanga njama na kutekeleza shambulio la bomu kwa kutumia gari wakati wa sherehe za uhuru wa Nigeria mwezi October mwaka 2010.

Mahakama hiyo imemkuta Henry Okah na hatia ya makosa 13 ya ugaidi ambayo yaliwasilishwa na upande wa mashtaka dhidi ya Okah.

Katika shambulio hilo watu kumi na mbili walipoteza maisha huku wengine zaidi ya thelathini na sita wakijeruhiwa kutokana na shambulio hilo.

Mbali na shambulio la mjini Abuja, Okah pia amepatikana na hatia ya kuhusika na mpango wa kutekeleza shambulio kwenye mji wa Warri tarehe 15 ya mwezi March mwaka 2010 ambapo mtu mmoja alipoteza maisha na wengine kumi na moja kujeruhiwa vibaya.

Katika hukumu ya mahakama hiyo, jaji alimuhukumu kifungo cha miaka 12 kwa kila kosa ambalo Okah alikuwa akituhumiwa kuhusika nayo.

Okah mwenyewe amekanusha kuhusika na matukio yote na kuongeza kuwa mashtaka dhidi yake yalichochewa kisiasa.