JAMHURI YA AFRIKA YA KATI-AFRIKA KUSINI-UN

Umoja wa Afrika AU, waifutia uanachama nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kufuatia mapinduzi yaliyofanyika nchini humo

Kiongozi wa waasi wa Seleka ambaye amejitangaza kuwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Michel Djotodia ametangaza kutotambua katiba ya nchi hiyo na kwamba ataongoza kwa kutumia mamlaka yake siku moja baada ya kuipindua Serikali ya rais Francois Bozize.

Kiongozi wa waasi wa Seleka, Michel Djotodia aliyejitangaza rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Kiongozi wa waasi wa Seleka, Michel Djotodia aliyejitangaza rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Reuters
Matangazo ya kibiashara

Tayari Jumuiya ya Kimataifa imelaani mapinduzi hayo ambapo Umoja wa Mataifa UN, umetangaza kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya waasi wa Seleka ambao wameingia madarakani huku waishuhudiwa wakiua watu wasio na hatia.

Djotodia mara baada ya kuingia Ikulu hapo jana ametangaza kutotambua katiba ya nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kulivunja bunge la nchi hiyo wakati huu ambao anasema anaunda Serikali ya mpito.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UN hapo jana liliitisha mkutano wa dharura kujadili kile kilichotokea nchini humo ambapo wamelaani kuuawa kwa wanajeshi 13 wa Afrika Kusini waliokuwa wakijaribu kuwazuia waasi hao wasiingie mjini Bangui.

Katika hatua nyingine Umoja wa Afrika AU, umetangaza kuiondolea uanchama kwenye Umoja huo nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kutangaza kutoitambua serikali inayoongozwa na waasi hao.

Rais wa Afrika Kusini Jackob Zuma amelaani kuuawa kwa wanajeshi wake na kueleza wasiwasi wake kuhusu wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao tayari wameripotiwa kufanyiwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na wapiganaji wa Seleka.

Rais aliyeondolewa madarakani Francois Bozize ameomba hifadhi nchini Cameroon baada ya kukimbilia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC baada ya waasi wa Seleka kuingia kwenye Ikulu yake.

Katika hatua nyingine wanajeshi wa Ufaransa walioko nchini humo ambao wanalinda uwanja wa ndege wa mjini Bangui, wamewaua raia wawili wa India katika kile inachodai kuwa walikuwa wakiingia kwa nguvu kwenye uwanja huo wakitumia gari lililodhaniwa kuwa ni lawaasi.