SYRIA-UMOJA WA NCHI ZA KIARABU-UN

Moaz: Marekani itekeleze kwanza ilichoahidi kwa waasi wa Syria

Ahmad Moaz al-Khatib kiongozi wa baraza la waasi wa Syria
Ahmad Moaz al-Khatib kiongozi wa baraza la waasi wa Syria REUTERS/Mohammed Dabbous

Kiongozi wa baraza la waasi wa Syria Moaz al-Khatibu licha ya kutangaza kujiuzulu nafasi yake alipewa nafasi kwenye mkutano wa Umoja wa Nchi za Kirabu, mkutano unaofanyika mjini Doha, Qatar.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye mkutano huo nchi wanachama zimewatambua rasmi viongozi wa baraza la waasi na kuwapa kiti cha kuiwakilisha nchi ya Syria kwenye mikutano ya Umoja huo kuanzia sasa, hatua ambayo imekosolewa na Serikali ya Damascus.

Mara baada ya kupewa nafasi ya kuwahutubia viongozi waliohudhuria mkutano huo, al-Khatibu ameitaka Serikali ya Marekani kutekeleza mpango wake wa kusaidia kutoa makombora ya kujihami kwa upande wa waasi ili kukabiliana na makombora ya Serikali.

Al-Khatibu amesema kuwa kuchelewa kutekelezwa kwa mpango huo ndiko ambako pia kumechangia atangaze kucahia nafasi yake kama kiongozi wa baraza la waasi wa Syria uamuzi ambao umeonekana kupokelewa vibaya na nchi wanachama.

Mkutano huo unafanyika bila ya kuwepo kiongozi wa Saudi Arabia mfalem Abdullah ambaye amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono harakati za waasi zilizoanza miaka miwili iliyopita pamoja na na rais wa Iraq Jalal Talabani.

Nchi ya Qatar ilikuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono waasi wa Syria ambapo imehakikisha nchi wanachama zinawakubalia waasi hao kuwa wawakilishi rasmi kwa nchi ya Syria ambapo pia wanatarajiwa kuchukua uongozi wa Umoja huo.

Nafasi ya Syria ilikuwa wazi toka Umoja huo utangaze kuifutia uanachama nchi hiyo baada ya kuanza kwa uasi nchini humo ambapo Umoja huo ulitangaza kutoutambua utawala wa rais Asad.

Toka kuanza kwa uasi nchini humo watu zaidi ya elfu sabini wameripotiwa kupoteza kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini humo.

Katika hatua nyingine Umoja wa Mataifa UN umetangaza kuwapunguza wafanyakazi wake mjini Damascus kwa muda mpaka pale hali ya usalama itakapoimarika, taarifa hiyo imetiwa saini na katibu mkuu wa Umoja huo Ban Ki Moon.

Uamuzi wa kupunguza wafanyakazi hao inakuja saa chache baada ya kuwepo taarifa kuwa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA na nchi za Kiarabu zimeanza kusafirisha silaha kwenda kwenye maeneo ambayo yanakaliwa na waasi.