MALI-UN

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, ataka kupelekwa vikosi vya kulinda amani nchini Mali

Katibu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki-Moon
Katibu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki-Moon REUTERS

Umoja wa Mataifa UN kupitia Katibu Mkuu wake Ban Ki Moon umesema zaidi ya wanajeshi wa kulinda amani elfu kumi na moja na mia mbili wanahitajika nchini mali ili kuchukua nafasi ya Majeshi ya Ufaransa yanayotarajiwa kuondoka nchini humo. 

Matangazo ya kibiashara

Ban ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kuwa walinzi wa amani wanahitajika haraka ili kwenda kushika doria nchini Mali baada ya majeshi ya Ufaransa kuendesha operesheni ya kusambaratisha Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanatawala Kaskazini.

Kauli hiyo ya Ban inakuja huku Makundi ya Kutetea Haki za binadamu nchini Mali kupitia Mohamed Issufu yakisema wananchi wamechoshwa na mateso waliyokutana nayo na kwa sasa wanahitaji amani pekee.

Baraza la Usalama liliidhinisha kupelekwa kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AU kwenda nchini humo kusaidiana na majeshi ya Ufaransa na yale ya nchi za magharibi mwa Afrika ECOWAS ambayo tayari yako nchini humo.

Ban ameongeza kuwa kikosi hicho cha wanajeshi kitalinda miji muhimu pekee na kwamba kutahitajika askari zaidi ambao watashika hatamu hata kwenye miji ambayo hakukuwa na upinzani mkali toka kwa wapiganaji wa kiislamu.

Licha ya kufurushwa kwenye miji mingi nchini humo wapiganaji wa kiislamu wamekimbilia kwenye maeneo ya milimani na kwenye jangwa la nchi hiyo linalopakana na nchi ya Algeria ambapo wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya wanajeshi wa Mali, Tchad na wale wa Ufaransa.

Licha ya katibu mkuu wa Ban Ki Moon kutaka kupelekwa kwa wanajeshi hao, watapelekwa nchini humo iwapo baraza la usalama litajiridhisha na hali ya usalama kwenye maeneo mengi nchini Mali.