DOHA-QATAR-SYRIA

Umoja wa nchi za Kiarabu waahidi kutoa ushirikiano zaidi kwa upinzani nchini Syria

Kiongozi wa baraza la Syria, Moaz al-Khatibu
Kiongozi wa baraza la Syria, Moaz al-Khatibu Reuters

Mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kirabu umeanza nchini Qatar katika Jiji la Doha ambapo umeshuhudia Upinzani nchini Syria ukitambulika rasmi kama Uongozi wa Taifa hilo na kuchukua nafasi ya serikali inayoongozwa na Rais Bashar Al Assad.  

Matangazo ya kibiashara

Mkutano huo umeng'oa nanga na kuhudhuriwa na wanachama wote wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu huku wakiutambua rasmi Muungano wa Upinzani kama Uongozi halali wa Syria na kudhihirisha Rais Assad hana nafasi tena.

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zimekutana kwenye mkutano wao ambao umeutambua Muungano wa Upinzani huku kukiwa na pendekezo la kutaka kuusaidia Upinzani kwenye vita yao dhidi ya Serikali ya Damascus.

Muungano wa Upinzani umewakilishwa na Ahmed Moaz Al Khatib aliyetangaza kujiuzulu wadhifa wake kama Kiongozi wa Muungano mapema juma hili lakini amerejea tena na kuomba wapatiwe msaada ili wafanikishe vita yao.

Al Khatib ambaye amechukua nafasi ya Rais Assad kwenye mkutano huo ametaka nchi wanachama za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kutopa ushirikiano ili waweze kulinda maeneo ambayo wanayashikilia.

Kiongozi huyo wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu hakuishi hapo bali akayageukia Mataifa ya Magharibi ya kuyataka nayo kuunga mkono juhudi wanazozifanya ili kuhakikisha wanaibuka washindi.

Kiongozi wa Qatar Hamad Bin Khalifa Al Thani ndiye ameongoza mkutano kwa siku ya kwanza akiwa mwenyeji ambapo amesema wakati umefika kwa Jumuiya hiyo kuusaidia Upinzani nchini Syria kushinda vita yake.

Al Thani ametaka wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuchangia jumla ya dola bilioni moja kuusaidia Upinzania ambao umetaka huruma ya nchi hizo kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya kifedha.

Vita nchini Syria vimeingia mwaka wa tatu huku takwimu za Umoja wa Mataifa UN zikionesha watu elfu sabini wamepoteza maisha huku wengine maelfu wakikimbia makazi yao na kuomba hifadhi ya ukimbizi katika nchi za Jordan na Uturuki.