KENYA-MOMBASA

Watu saba wauawa kwenye shambulio la risasi mjini Mombasa, Kenya

Wafuasi wa kundi la MRC ambao kundi lao linahusishwa na mashambulizi ya hii leo
Wafuasi wa kundi la MRC ambao kundi lao linahusishwa na mashambulizi ya hii leo Reuters

Watu saba wameripotiwa kuuawa akiwemo polisi mmoja huku wengine wakijeruhiwa kufuatia mapambano ya polisi na watu waliokuwa na silaha waliposhambulia ukumbi mmoja wa Casino mjini Mombasa. Mkuu wa Polisi mjini Mombasa Aggrey Adoli amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa kundi la watu waliokuwa na silaha walivamia ukumbi huo na kuanza kuwafyatulia watu risasi kabla ya kukabiliana na Polisi ambapo askari mmoja alipoteza maisha.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa kamanda Adoli, amesema kuwa wanaodhaniwa kuwa ni kutoka kundi la Mombasa Republic Council MRC ambalo linataka pwani kujitenga na Kenya ndio waiotekeleza shambulio hilo kwenye mji wa Malindi ambao pia hutumiwa kama mji wa utalii.

Kamanda Adoli amesema kuwa tukio hilo limetokea alfajiri ya hii leo maajira ya sanane za usiku wakati wananchi wa mji wa Malindi walikuwa wakiendelea kuburudika kwenye ukumbi huo.

Polisi wamesema kuwa kundi hilo la watu linakadiriwa kufikia watu mia moja ambao wote walikuwa na silaha ambapo wakati wakitekeleza shambulio hilo polisi wanne walikuwa kwenye doria jirani na eneo la tukio na kuanza kukabiliana nao.

Shambulio hilo limeendelea kuzusha hofu zaidi kwa wakazi wa mji wa Mombasa na maeneo mengine kufuatia kundi la MRC kufanikisha mara kwa mara kutekeleza mashambulizi ambayo yanagharimu maisha ya watu.

Hivi karibu nchi ya Marekani iliwaraka raia wake kuwa makini wanapotembelea mji wa Mombasa na kwamba kutokana na hali ya usalama kutokuwa ya kuridhisha iliwataka kuwa makini wakati wote.

Mji wa Mombasa hasa eneo la Malindi limepoteza mvuto kwa watalii wengi ambao walikuwa wakitembelea mji huo kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi ya kushtukiza yanayofanywa na wafuasi wa kundi la MRC.