DRC-UN

UN: Yatoa makataa ya wiki moja kwa DRC kuwakamata wanajeshi wake wanaotuhumiwa kwa ubakaji

Wanawake na watoto nchini DRC ndio wanatajwa kuwa waathirika wakubwa wa vitendo vya ubakaji
Wanawake na watoto nchini DRC ndio wanatajwa kuwa waathirika wakubwa wa vitendo vya ubakaji Reuters

Umoja wa Mataifa UN, umeipa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC muda wa wiki moja kuhakikisha inachukua hatua madhubuti kukabiliana na vitendo vya ubakaji vinavyoripotiwa mashariki mwa nchi hiyo. 

Matangazo ya kibiashara

Umoja huo umeitaka Serikali ya rais Joseph Kabila kuchukua hatua dhidi ya makundi mawili ya wanajeshi wa Serikali yanayopigana mashariki mwa nchi hiyo ambapo wametajwa kutekeleza vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake na watoto.

Makundi hayo ya mawili ya wanajeshi wa Serikali kwenye mji wa Goma yanaelezwa kutekeleza vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake 126 huku Serikali ya nchi hiyo ikishindwa kuchukua hatua stahiki za kuwakamata waliotajwa kuhusika na vitendo hivyo.

Mashirika ya kiraia kwenye mji wa Goma yalitoa ripoti hivi karibuni ikiwataja wanajeshi wa Serikali waliogawanyika kwenye vikundi kutekeleza vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake huku Serikali licha ya kupata taarifa imeshindwa kuwakamata askari wake na kuwafikisha kwenye vyombo husika.

Makataa hiyo ya Umoja wa Mataifa imetolewa na mkuu wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja huo, Herve Ladsous ambaye alikuwa na mkutano na waziri wa mambo ya nje wa DRC Raymond Tshibanda kwenye makao makuu ya Umoja huo.

Mkutano huo umefanyika wakati ambapo nchi wanachama za baraza la usalama la Umoja huo wanakutana kuoiga kura kuidhinisha mpango maalumu wa kupelekwa kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja huo mashariki mwa Jamhuri ya Kideomokrasia ya Kongo.

Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika ya kutetea haki za binadamu yameonesha wasiwasi wao kuhusu hali ya machafuko inayoendelea mashariki mwa nchi hiyo ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la vitendo vya ubakaji vinavyofanywa na wanajeshi wa Serikali pamoja na makundi ya waasi.

Juma moja lililopita Umoja huo uliiandikia barua Serikali ya Kongo ikitishia kuacha kufanya kazi na wanajeshi wake ambao wametajwa kuhusika na vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake na watoto.