CYPRUS-EU-ECB-IMF

Wananchi wa Cyprus bado waendelea kukabiliwa na hali ngumu kiuchumi

Moja ya benki ambayo ilitangazwa kufilisiwa na Serikali
Moja ya benki ambayo ilitangazwa kufilisiwa na Serikali REUTERS

Benki ya Cyprus imetangaza vikwazo ambavyo vimetawekwa kwenye sekta ya kifedha nchini humo na ambavyo vitadumu kwa kipindi cha mwezi mmoja kabla ya hali kurejea kama ilivyokuwa awali lengo likiwa ni kulinda uchumi wa Taifa hilo. 

Matangazo ya kibiashara

Kauli hiyo imekuja huku Benki zikifunguliwa kwa mara ya kwanza hiyo jana baada ya kufungwa kwa kipindi cha karibu majuma mawili kutokana na uwepo wa mdodoro wa uchumi ualiokuja baada ya wananchi wengi kutoa fedha zao kukwepa kukatwa kodi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Cyprus Ioannis Kasoulides amejitokeza na kueleza hali itarejea kwa mwendo wa taratibu na hivyo kuwataka wananchi kuwa watulivu kwa kipindi hiki cha mwezi mmoja.

Wakati Serikali ikitangaza hatua hizo, bado wananchi wa Cyprus wamepanga kufanya maandamano zaidi kupinga mpango wa nchi yao kukubali matakwa ya Umoja wa Ulaya na shirika la fedha duniani ili nchi yao ipatiwe mkopo.

Wananchi bao wanapinga kutozwa kodi kwa fedha zao ambazo ziko kwenye mabenki nchini humo jambo ambalo liliwafanya waziondoe fedha zao kwenye benki kukwepa kulipa kodi hizo.

Hapo jana pia Serikali ilitangaza viwango maalumu kwa wananchi kutoa kwenye akaunti zao pamoja na fedha ambazo wageni wanaruhusiwa kusafiri nazo wakiwa wanatoka nje ya taifa hilo.

Mpango huo wa Serikali pia utashuhudia sekta ya ajira ikiathirika kutokana na makampuni mengi kulazimika kupunguza wafanyakazi ili kukabiliana na hali ngumu ya kifedha ambayo imtokana na kuidhinishwa kwa mpango huo.