KOREA KASKAZINI

Marekani yasema iko tayari kuzungumza na Korea Kaskazini kuhusu Nyuklia

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema Marekani iko tayari kuzungumza na Korea Kaskazini kuhusu mpango wake wa Nyuklia kwa lengo la kupata suluhu la amani ya kudumu katika eneo la Korea. 

Matangazo ya kibiashara

Kerry ameongeza kuwa Pyongyang ina jukumu la kuhakikisha kuwa inatekeleza maazimio ya Kimataifa iliyokubali kuhusu mradi wa Nyuklia ambao umeonekana kuwa hatari kwa dunia.

Wakati Kerry akiyasema hayo, dunia inasubiri kuona ikiwa Korea Kaskazini itafanya jaribio la zana zake za Nyuklia siku ya Jumatatu, siku ambayo inaadhimisha kumbukumbu ya aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo hilo Kim Il-Sung.

Waziri Kerry amekuwa nchini Korea Kusini, China na Japan kuonesha ushikamano na mataifa hayo yanayopakana na Korea Kaskazini .

Kerry ameendelea kusema kuwa shambulizi lolote kwa jirani zake ni hatari sana pia kwa watu wake na kuongeza kuwa Marekani iko tayari kujilinda pamoja na washirika wake.

China ambayo inaangaziwa kama taifa linaloweza kusaidia kumaliza kwa vitisho vya Korea Kaskazini imemwahidi John Kerry kuwa itashirikiana naye ili kupunguza hali ya wasiwasi katika eneo la Korea.

Korea Kaskazini katika siku za hivi karibuni imeendelea kusisitiza kuwa itafanya majaribio ya zana zake za kivita na pia kuishambulia Korea Kusini, Japan na Marekani.

Vitisho hivyo vimedhoofisha uhusiano kati ya Korea Kaskazini na Kusini na hata kufungwa kwa kampuni ya pamoja huku Marekani ikiweka tayari mitambo ya kuzuia mashambulizi yoyote ya Nyuklia .