VENEZUELA

Upinzani nchini Venezuela wataka kura kuhesabiwa tena

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Henrique Capriles anataka Tume ya uchaguzi nchini humo kurudia tena zoezi la kuhesabu  zilimpa  ushindi mwembamba rais Nicolas Maduro.  

Matangazo ya kibiashara

Tume ya Uchaguzi nchini humo siku ya Jumatatu  ilimtagaza Nicolas Maduro mshindi wa uchaguzi huo baada ya kupata ushindi mwembamba wa asilimia 50 nukta 7 dhidi ya Capriles aliyepata asilimia 49 nukta 1.

Capriles amekataa kuyatambua matokeo hayo na kusema Maduro hakushinda uchaguzi huo kwa kile anachosema udanganyifu wa hali ya juu ulitokea wakati wa kupiga kura.

Kiongozi huyo wa upinzani ameongeza kuwa kuna zaidi ya visa 300,000 vya wizi wa kura vilivyotokea na uchunguzi wa kina unastahili kufanyika ili kupata ukweli.

Tume ya Uchaguzi nchini humo inasema kuwa matokeo iliyotangaza ni ya kweli na haiwezi kuyabadilisha.

Naye rais Maduro akiwahotubia wafuasi wake katika Ikulu ya rais jijini Caracas baada ya kutangazwa mshindi, amesema ameshinda kihalali na kisheria.

Aidha, amesisitiza  kuwa ushindi wake umeonesha wazi kuwa bado watu wa Venezuela  wanampenda Marehemu Hugo Chavez ambaye alifariki dunia mwezi Machi mwaka huu.

Rais Maduro amewaambia wananchi wa Vanezuela kuwa amezungumza na kiongozi wa upinzani Capriles na kumhakikishia kuwa amekubali kuhesabiwa upya kwa kura hizo huku akitoa wito kwa wapinzani kuungana naye kuendelea kulijenga taifa hilo.

Maduro ataapishwa tarehe 19 mwezi huu na kuhudmu kwa muda wa miaka sita hadi mwezi Januari mwaka 2019 kabla ya kufanyika tena kwa uchaguzi mwingine.