VENEZUELA

Tume ya Uchaguzi nchini Venezuela yathibitisha ushindi wa Maduro

Tume ya Uchaguzi nchini Venezuela imemthibitisha Nicolas Maduro kuwa mshindi halisi wa uchaguzi wa urais nchini humo kwa kupata ushindi mwembamba wa asilimia 50 nukta 7 dhidi ya mpinzani wake Henrique Capriles aliyepata asilimia 49 nukta1.

Matangazo ya kibiashara

Tangazo hilo limesababisha maandamano makubwa na makabiliano kati ya wafuasi wa Capriles na polisi jijini Caracas.

Polisi wamekuwa wakitumia mabomu ya kutoa machozi kuwasambaratisha waandamanaji hao wengi wao wakiwa wanafunzi waliofika katikati ya jiji na kuanza kufanya uharibifu wa mali.

Awali, kiongozi wa upinzani Capriles aliomba tume hiyo kutomthibitisha Maduro kama mshindi na kuonya kuwa ikiwa ingetokea hivyo basi angeongoza wafuasi wake hadi katika makao makuu ya tume hiyo kupinga matangazo hayo.

Capriles amekataa kuyatambua matokeo hayo na kusema Maduro hakushinda uchaguzi huo kwa kile anachosema udanganyifu wa hali ya juu ulitokea wakati wa kupiga kura.

Kiongozi huyo wa upinzani ameongeza kuwa kuna zaidi ya visa 300,000 vya wizi wa kura vilivyotokea na uchunguzi wa kina unastahili kufanyika ili kupata ukweli.

Tume ya Uchaguzi nchini humo inasema kuwa matokeo iliyotangaza ni ya kweli na haiwezi kuyabadilisha.

Naye rais Maduro akiwahotubia wafuasi wake katika Ikulu ya rais jijini Caracas baada ya kutangazwa mshindi, alisema ameshinda kihalali na kisheria.

Maduro ataapishwa tarehe 19 mwezi huu na kuhudmu kwa muda wa miaka sita hadi mwezi Januari mwaka 2019 kabla ya kufanyika tena kwa uchaguzi mwingine.