MALI-UFARANSA-UN

Ban: Uchaguzi mkuu wa Mali uheshimike hata kama utakuwa na mapungufu

Rais wa Ufaransa, François Hollande akiwa na mgeni wake rais wa Mali, Dioncounda Traore
Rais wa Ufaransa, François Hollande akiwa na mgeni wake rais wa Mali, Dioncounda Traore REUTERS/Ian Langsdon/Pool

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa UN, Ban Ki Moon ametaka matokeo ya uchaguzi mkuu wa urais utakaofanyika nchini Mali mwishoni mwa mwezi yaheshimiwe hata kama zoezi la upigaji kura litagubikwa na kasoro. 

Matangazo ya kibiashara

Katibu mkuu Ban ametoa kauli hiyo kufuatia tume ya taia ya uchaguzi nchini Mali kukosolewa kutokana na kuonekana kutokuwa tayari kuandaa uchaguzi mkuu tarehe 28 ya mwezi huu kutokana na sababu mbalimbali.

Ban ameyasema hayo ikiwa ni siku moja imepita baada ya kuhudhuria sherehe za kitaifa nchini Ufaransa siku ya Jumapili, ambapo amesema ni lazima matokeo ya uchaguzi wa Mali yaheshimiwe licha ya mapungufu yatakayojitokeza.

Siku ya Jumapili, katibu mkuu Ban alikutana na rais wa mpito wa Mali, Dioncounda Traore na rais wa Ufaransa, Francois Hollande ambapo kwenye mazungumzo yake na viongozi hao, wamekubaliana kuisaidia nchi ya Mali kuandaa uchaguzi uliokuwa huru na haki.

Hofu zaidi imeendelea kutanda kwenye jimbo la Kidal kaskazini mwa nchi hiyo ambako kumekuwa na machafuko kati ya waasi wa kiislamu na wanajeshi wa Serikali wakati huu ambapo zaidi ya watu laki tano hawana makazi ya kuishi.

Hata hivyo siku ya Jumamosi waziri wa mambo ya nje wa Mali, Tieman Coulibaly amesema kuchelewesha kufayika kwa uchaguzi mkuu ncbhini humo kutasababisha hali ya kisiasa kuwa mbaya zaidi.

Katika hatua nyingine rais wa Ufaransa, Francois Hollande amesema kuuawa kwa raia wake waliokuwa wametekwa na wapiganaji wa Al-Qaeda kaskazini mwa Mali hakutaifanya nchi hiyo kusitisha vita dhidi ya ugaidi na kwamba damu ya raia wake italipizwa.