ZIMBABWE

Upinzani walalama nchini Zimbabwe kuhusu dosari zilizoshuhudiwa siku ya Jumapili wakati polisi wakipiga kura

Msururu wa askari polisi wa Zimbabwe walioshiriki kupiga kura siku ya Jumapili
Msururu wa askari polisi wa Zimbabwe walioshiriki kupiga kura siku ya Jumapili Reuters

Maandalizi ya uchaguzi mkuu cnhini Zimbabwe yamekumbwa na dosari kufuatia hapo jana baadhi ya karatasi za kupigia kura kushindwa kufika kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura ambako askari na wanajeshi walikuwa wakipiga kura za awali. 

Matangazo ya kibiashara

Dosari hizo zinajitokeza wakati zikiwa zimebaki wiki chache kabla ya kushuhudia wananchi wa Zimbabwe wakishiriki zoezi la upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu wa Urais.

Siku ya Jumapili tume ya taifa ya uchaguzi ilitangaza ndio siku ambayo wafanyakazi wa vyombo vya usalama watapiga kura kwenye zoezi ambalo lilikumbwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosekana kwa karatasi za kupigia kura na kuchelewa kufunguliwa kwa vituo.

Waziri mkuu Morgan Tsvangirai ambaye anawania urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha MDC, amesema kilichoshuhudiwa Jumapili hii ni ishara tosha kuonesha kuwa tume ya taifa ya uchaguzi haiko tayari kwa uchaguzi mkuu wa tarehe 31 mwezi huu.

Kiongozi huyo ameongeza kuwa, kuchelewa kufika kwa karatasi za kupigia kura ni mwanzo unaonesha kuwa uchaguzi wa mwaka huu pia hautakuwa huru na wa haki kwakuwa tayari tume imeonesha kutokuwa tayari kwa uchaguzi.

Chama hicho kimepanga kuwasilisha pingamizi mahakamani hii leo kupinga asakri wengi kushiriki zoezi la uchaguzi, kwa kile inachodai ni njama za rais Mugabe kutaka kupata kura nyingi za askari.

Kwa mujibu wa tume ya taifa ya uchaguzi nchini Zimbabwe ZEC imesema kuwa zaidi ya askari elfu 87 walijiandikisha kupiga kura na kushiriki kwenye zoezi la siku ya Jumapili ya tarehe 14 ya mwezi huu.

Baadhi ya askari waliamua kuondoka kwenye vituo vya kupigia kura baada ya karatasi kuchelewa kufika kutokana na hadi kufika mchana karatasi zilikuwa bado zikirudifishwa.