SUDAN-NIGERIA

Ikulu ya Nigeria yaeleza kwanini haitamkamata rais wa Sudan, Omar al-Bashir

Rais wa Sudan, Omar al-Bashir akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Abuja, Nigeria siku ya Jumapili
Rais wa Sudan, Omar al-Bashir akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Abuja, Nigeria siku ya Jumapili Reuters

Ikulu ya Nigeria hii leo imetoa taarifa kueleza ni kwanini haitamkamata rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashiri ambaye yuko nchini humo kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika kuhusu afya.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ya rais Goodluck Jonathan inasema kuwa rais Bashir hayuko nchini Nigeria kwa mwaliko wa Serikali lakini anahudhuria mkutano huo kwa mwaliko wa Umoja wa Afrika ambao ndio waandaaji wake.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa haiwezi kuingilia maamuzi ya AU na kwamba angekuwa amealikwa na nchi hiyo pengine wangeweza kumkata rais Bashir.

Nchi ya Nigeria ni moja kati ya mataifa yanayoitambua mahakama ya ICC na walitia saini kuitambua mahakama hiyo na wanaowajibu wa kufanya hivyo, mmoja wa wanaharakati alisikika akisema.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini humo hii leo wamewasilisha kesi kwenye mahakama kuu kuishinikiza Serikali kutekeleza mkataba iliotiliana saini na mahakama ya ICC kwa kumkamata al-Bashir.

Godfrey Musila ni mchambuzi wa masuala ya siasa akiwa Nairobi nchini Kenya, kwenye mahojiano yake na idhaa ya kiswahili ya RFI ya Dar es Salaam Tanzania, amesema kuwa suala hilo liko kisiasa zaidi na ndio maana Nigeria haitaweza kutekeleza.

Musila ameongeza kuwa licha ya Nigeria kuitambua mahakama ya ICC, lakini maazimio yaliyofikiwa na viongozi wa Afrika kuhusu kutoshirikiana na mahakama hiyo pia kumechangia Serikali ya Nigeria kutomkamata rais Bashir.

Rais Bashiri anahudhuria mkutano wa afya ulioandaliwa na Umoja wa Afrika AU na aliwasili mjini Abuja siku ya Jumapili ambapo mkutano huo unafanyika Jumatatu hii na kesho Jumanne.